Friday, July 18, 2008

neno ufisadi lazua maneno

Mzalendo Safari,
Salaam aleikum,

Nimesoma habari kama mara mbili hivi katika magazeti ya hapo kwetu zinazomnukuu katibu mkuu wa CCM, Mhe Makamba akiwaeleza watu kuwa maana ya neno 'ufisadi' ni ile tu iliyo katika kamusi ya Kiswahili (ninajua kamusi anayonukuu ni ile iliyochapishwa mwaka 1981 na kurudiwa katika miaka michache iliyopita).

Ninaomba unifikishie ujumbe wangu huu kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), (maana sioni kama wana tovuti wala anwani ya baruapepe), kwamba kama kitengo cha serikali kilicho na wajibu wa kushauri serikali na viongozi kama Makamba kuhusu matumizi ya lugha, wamweleweshe kuhusu tabia ya lugha (kwamba huibuka, hukua, hutanuka kama mti na matawi, na wakati mwingine huweza ikavia, au ikafa), pili wamweleweshe kuhusu maana ya kamusi (kamusi sio biblia au msaafu).

Kuhusu utunzi wa kamusi, hususan ule wa kimapokeo huwa tuna msemo mmoja kwamba "siku kamusi inapochapishwa tayari inakuwa imepitwa na wakati." Hii ni kutokana na ukweli kuwa lugha huwa haikai kusubiri kamusi. Ukiwauliza watumiaji wa Kiswahili leo hii maana ya neno 'fisadi' watakwambia bila kusita maana yake hai.

Hiyo ambayo Mhe Makamba anainukuu hata kwa watoto wa vidato vya tano na sita ni maana butu au mfu. Ninafikiri hapa ipo haja ya BAKITA kutimiza wajibu wao.

Ninatanguliza shukurani na asante sana kwa kazi nzuri ya kutuhabarisha kwa mtindo wa blogu.

Charles Bwenge
Chuo Kikuu cha Florida
Gainesville,
Florida,
USA.

No comments: