Saturday, July 5, 2008

Ahadi zote za Rais Kikwete
Miundombinu kutekelezwa-
Dk Kawambwa

WIZARA ya Maendeleo ya Miundombinu imesema ahadi alizotoa Rais Jakaya Kikwete kwa nyakati tofauti zikiwamo za wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 ni amri, zote zitatekelezwa.Waziri wa wizara hiyo,Dk. Shukuru Kawambwa(Pichani)amesema bungeni kuwa serikali imedhamiria kutekeleza ahadi hizo, ukiwamo ujenzi wa barabara kama alivyoahidi Rais.

Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, Serikali ya Awamu ya Nne imejipanga kuhakikisha kuwa ahadi hizo zinatekelezwa sanjari na ahadi za kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005.Dk. Kawambwa alilieleza Bunge kuwa baadhi ya ahadi zimeanza kutekelezwa kulingana na uwezo wa bajeti na kwamba serikali itajitahidi kupata fedha kadri itakavyoweza.Alisema serikali imeanza kutathmini fursa nyingi za kupata fedha za ujenzi wa miundombinu,ikiwamo mikopo ya muda mrefu na kwamba, fursa hizo zitaainishwa katika sera maalumu.

Aliyasema hayo wakati akijibu hoja za wabunge wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Matumizi kupitia vifungu vya bajeti ya Wizara hiyo iliyopitishwa Alhamisi saa mbili usiku.Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali,John Cheyo,alisema tatizo si fedha, bali menejimenti ya miradi ya ujenzi wa miundombinu.Alisema fedha zinazopangwa kwa ujenzi wa barabara zinatumika vibaya na gharama zimekuwa zikipanda bila sababu za msingi.Habari na Mdau Msimbe Lukwangule

No comments: