Thursday, July 3, 2008

Mkutano wa Wajasiriamali
nchini Uingereza..
Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Hon Mwanaidi Maajar akitoa nasaha zake
kwenye mkutano wa wajasirimali nchini Uingereza.

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Kusaidia Mazingira ya Uwekezaji Afrika
(Investment Climate Facility for Africa),Bw. Omar Issa akiongea na wadau mbalimbali kwenye mkutano wa wajasirimali nchini Uingereza,kushoto kwake ni Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza Hon Mwanaida Maajar.Kulia ni Mwenyekiti wa jumuiya ya watanzania nchini humo Abuu Faraji.
Mwenyekiti wa jumuiya ya Watanzania nchini Uingereza Abuu Faraji kwenye mkutano wa wajasirimali uliyofanyika nchini humo.-------------
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Kusaidia Mazingira ya Uwekezaji Afrika (Investment Climate Facility for Africa), Bw. Omar Issa amekutana na Wajasiriamali wa Kitanzania waishio Uingereza na kuwapa changamoto ya kuanzisha biashara nyumbani.Katika Mkutano uliofanyika jana katika jengo la Ubalozi wa Tanzania, London Uingereza (Tanzania House), Bw. Issa aliainisha fursa nyingi za biashara zilizopo Tanzania baada ya Serikali kufungua milango zaidi ya uwekezaji na kupatikana kwa wawekezaji wakubwa wa Kimataifa.

Akifafanua zaidi mtaalam huyo alisema hivi sasa takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania inahitaji zaidi biashara za uwezo wa kati (medium enterprises) ili kuziba pengo kubwa kati ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo. Alisema ili kuendelea zaidi kiuchumi, makampuni makubwa yanahitaji sana makampuni ya kati kwa ajili ya kutengeneza mali ghafi, kuzalisha nguvu kazi na kutoa ushauri wa kitaaluma. Katika Mkutano huo ulihudhuriwa na watanzania zaidi ya 30, Bw. Issa aliwashauri wajasiriamali hao kubuni miradi mbalimbali itakayowawezesha kupata mikopo kwenye benki za Tanzania ili kuweza kuanzisha biashara huko nyumbani. Aliwapa changamoto kuangalia fursa za biashara za huduma na ushauri wa kitaaluma.

Alisema benki nyingi hivi sasa nchini Tanzania zinawatafuta wenye miradi ya uhakika ili kuwakopesha mitaji ya kufanya biashara nchini humo.Alisema kwa elimu, upeo na uzoefu waliokuwa nao, wajasiriamali hao wanaweza kuanzisha miradi mizuri itakayowezesha kuinua uchumi wa Tanzania.Kwa mafanikio zaidi,Bw. Issa amewashauri wajasiriamali hao kujiunga katika vikundi ili kuweza kujumuisha utaalam na mitaji ya msingi ya kuanzisha miradi hiyo.

Alisema biashara nzuri inahitaji utafiti wa soko,udhibiti na shauku ya maendeleo zaidi
Katika maswali yao kwa mtoa mada,Wajasirimali hao walipenda kufahamu mipango zaidi ya Serikali kuondoa urasimu.Bw. Issa aliwaambia kwamba wakati Serikali inaendelea na hatua mbalimbali kurekebisha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini Tanzania, ni vyema Watanzania hao pia kutimiza wajibu wao badala ya kukaa tu kusubiri Serikali kufanya kila kitu.

Alifafanua kwamba Watanzania walioko nje ya nchi wana uwezo mkubwa sana wa kubadilisha mazingira ya uwekezaji kama watarudi nyumbani na kuingiza utamaduni mpya wa kikazi.
Awali akimkaribisha mtoa mada, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar alisema kwamba Ubalozi hivi sasa unafanya jitihada za kuwaunganisha wajasiriamali wa Kitanzania wa ngazi zote walioko Uingereza ili kuwashirikisha kikamilifu na Baraza la Biashara la Tanzania (Tanzania Business Council). Bw. Issa yupo London kwa ajili ya Mkutano wa Uwekezaji wa Africa (Africa Business Forum 2008) ulioandaliwa na Commonwealth Business Forum.

No comments: