Saturday, July 5, 2008

Kinondoni Biafra: Angalia Tofauti,1988 Na 2008!


Mwezi kama huu mwaka 1988 nilipiga picha hiyo ya juu. Nilikuwa tu na mapenzi ya kupiga picha na kuweka kumbukumbu. Picha zangu nyingi hazikupata nafasi ya kuchapwa magazetini. Sikujua kuwa iko siku picha hizo ziingekuwa na maana kubwa katika kulinganisha tofauti ya wakati na mabadiliko kupitia teknolojia hii ya blogu. Hakika, jambo hili limenihamasisha kuendelea kupekua kwenye maboksi yangu kuzitafuta picha za zamani. Limenihamasisha pia kuendelea kupiga picha na kuzihifadhi vema hata kama hazitumiki kwenye magazeti au kwenye blogu. Naamini siku moja kuna mtu atazitumia kwa madhumuni kama haya ya sasa.
Turudi kwenye picha. Hapo juu utaona njia ndogo ya miguu ambayo niliipita sana kwenda dukani kwa Tarimo hapo kulia kwenye maghorofa ya NBC ya zamani. Hapo kwenye kinjia hicho kulikuwa na shamba kubwa la mpunga. Hivyo, nilikuwa nakatisha shambani kwa mtu. Nakumbuka wakati wa mvua kulikuwa na chura wengi sana maeneo ya Kinondoni Biafra. Kama unavyoona,watu walikuwa wa kuhesabika, hivyo hivyo magari, wakati fulani tuliweza kuhesabu magari yanayopita Morocco Road!
Picha ya chini nimeipiga leo asubuhi katika engo ile ile niliyosimama mwaka 1988. Inanikumbusha mbali sana, na hakika tumetoka mbali!

No comments: