Friday, May 2, 2008

Wahisani waipa ukomo serikali kutekeleza ripoti ya Richmond

Na Tausi Mbowe (Mwananchi), Bagamoyo
WAHISANI wameitaka serikali kuhakikisha inatekeleza mapendekezo ya ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, iliyoundwa kuchunguza mchakato wa zabuni ya umeme ulioipa ushindi Kampuni ya Richmond ya Marekani, ifikapo Juni, mwaka huu la sivyo hawatachangia bajeti ya 2008/9.

Uamuzi huo wa Wahisani ulielezwa jana na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo alipokuwa akitoa mada katika semina ya Mafunzo kwa Wabunge wa Kamati za Bunge za Hesabu iliyokuwa ikifanyika mjini hapa.

Mkullo alikiri kwamba ufisadi katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) na katika zabuni ya Richmond, umeitikisa nchi na dunia, hali iliyosababisha wahisani kuonyesha nia ya kutoisaidia Tanzania katika bajeti yake, lakini baada ya mazungumzo na serikali wahisani hao wamerejesha tena nia hiyo.

Mkullo alisema wahisani hao waliridhika na jinsi Rais Jakaya Kikwete alivyoshughulikia ufisadi katika EPA kwa kuchukua hatua iliyosababisha kuvuliwa madaraka aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Ballali, hivyo kuonyesha nia yao tena ya kuisaidia Tanzania.

Hata hivyo, Waziri Mkullo alisema baada ya mazungumzo na wahisani hao, walikubaliana

kuhakikisha kuwa mapendekezo yote yaliyopo katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, chini ya uenyekiti wa Dk Harrison Mwakyembe, yanatekelezwa ifikapo Juni, mwaka huu.

Alisema ili kuhakikisha jambo hilo linatekelezeka, serikali pamoja na wahisani hao, wameweka utaratibu wa kukutana kila mwisho wa mwezi ili kupeana maendeleo na kwamba, kikao cha kwanza kilikuwa kifanyike jana.

Kutokana na kikao hicho, Waziri Mkullo ambaye jana alikuwa akitoa mada katika semina ya Mafunzo kwa Wabunge wa Kamati za Bunge za Hesabu iliyokuwa ikifanyika mjini hapa, alishindwa kuendelea mpaka mwisho wa semina hiyo na kuomba arudi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kukutana na baadhi ya mabalozi wa nchi mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano waliojiwekea.

''Baada ya masakata yote haya ya ufisadi, tulikaa na wafadhili tukaweka action plan (ratiba ya utekelezaji) ili kuwatoa hofu wafadhili wetu kuwa mambo haya hayatatokea tena. Hivyo, tulikubaliana kuhakikisha upande wetu wa serikali unatekeleza mapendekezo yote ya ripoti ya Dk Mwakyembe, kwa upande wao waliomba wakutane na Waziri wa Fedha kila mwezi ili kuwapa feedback (mrejesho) ya nini kilichofanyika katika kutekeleza hilo,'' alisema Waziri Mkullo.

Alisema tayari wahisani wameshamuandikia barua kujua utekelezaji wa mapendekezo hayo yamefikia katika hatua gani na kama inatekelezeka hivyo katika kikao hicho cha jana alikuwa akienda kuwapa maelezo namna serikali ilivyotekeleza mapendekezo hayo.

Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge, ni pamoja na kuitaka serikali kuwawajibisha wahusika, kulieleza Bunge ilikofikia na kuangalia uwezekano wa kusitisha mkataba wa Kampuni ya Dowans iliyonunua hisa za Kampuni ya Richmond.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkullo alisema serikali ina mpango wa kupeleka sheria bungeni ili kuweza kuwashughulikia wote wanaojihusisha na matumizi mabovu ya fedha za umma.

Alisema katika sheria hiyo, watakaobainika kujihusisha kwa namna yoyote na matumizi mabaya ya fedha za umma, watapewa adhabu kali kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, waziri huyo hakuwa tayari kutaja adhabu hizo ingawa alisema adhabu zote zimeainishwa katika sheria hiyo.

“Wote watakaopatikana na hatia ya matumizi mabaya ya pesa, wanaojihusisha na uvujaji wa pesa za serikali na umma kinyume cha taratibu za nchi watawajibika kwa,mujibu wa sheria, hizi ni pesa za umma. Wahisani wanachangia asilimia 40 ya bajeti yetu asilimia 60 inayobaki ni kodi zetu, ni lazima wawajibishwe kwa mujibu wa sheria na kuchukuliwa adhabu kali kwa kosa la kutafuna pesa zetu,” alisema Waziri Mkullo.

Pia alisema sheria zote za mrabaha zinatarajiwa kubadilishwa kutokana na baadhi ya mashirika ya umma kutolipa gharama za mrabaha.

Alisema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Wete, Mwadini Abbas Jecha aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kutokana na baadhi ya mashirika ya umma kutolipa mrabaha huku akitoa mfano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa nchini (TANAPA) na Hifadhi ya Mbunga za Wanyama ya Ngorongoro.

Wakati huo huo, Mbunge wa Igalula, Tatu Ntimizi, amepasua bomu kwa kumbana Waziri Mkullo kutoa ufafanuzi kwa nini Ofisi ya Waziri Mkuu, iliagiza magari ya kifahari ambayo yaligharimu kiasi kikubwa cha fedha na bila kufanya utafiti kujua yalihitajika magari gani badala yake magari hayo yaliachwa na kuagizwa aina nyingine ya magari.

''Hii ni mianya ya rushwa, ni aibu hata ofisi za wakuu wa nchi na maafisa wake, wanajitengenezea mianya na mazingira ya fedha kuliwa na si matumizi halisi kwanini? Tunaomba mheshimiwa waziri utujibu katika suala hili,'' alisema Ntimizi na kuongeza:

''Ofisi ya Waziri Mkuu iliagiza magari ya kifahari aina ya Lexus. Lakini muda mfupi baada ya magari hayo kufika tu, ikagundulika kuwa hayafai kwa ajili ya Waziri Mkuu na ndipo ofisi hiyo ilipoamua kuagiza aina nyingine ya magari kwa jili ya kiongozi huyo. Wewe ndio waziri wetu tunahitaji majibu katika hili, hapa ukaguzi unaendaje?''.

Alisema taasisi za serikali zimekuwa na matumizi mabaya ya fedha na kumtaka waziri kueleza kama ukaguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameliona hilo na hatua gani zimechukuliwa.

Ntimizi pia alisema serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, imenunua dawa mbalimbali, zikiwamo za mabusha na kuzipeleka sehemu ambazo hazina matatizo ya ugonjwa huo, huku akitoa mfano wa Tabora ambapo alidai zimepelekwa kwa wingi.

''Hii ni aibu nchi ina matatizo mengi watu wachache wanapitisha ununuzi wa dawa kama ya mabusha na kupeleka sehemu ambazo hazina matatizo hayo huku wananchi wakila mlo mmoja na wenyewe wanajiwekea mazingira ya kula pesa,'' alisema Ntimizi.

Kikao hicho cha wabunge ambacho kimekaa kwa siku tatu mjini hapa, jana kilionekana kuwa mwiba kwa serikali baada ya wabunge kumbana waziri huyo kwa maswali lukuki na kumtaka ajibu maswali hayo kwa maandishi, ili kuepuka kutoa majibu kirahisi na yasiyokidhi.

Kabla ya kujibu, Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo alimtahadharisha Waziri Mkullo kuwa kikao hicho si legelege kwa kuwa sasa wabunge wamekomaa na kwamba, wamehitimu na wanataka majibu ya kina.

Kabla ya kujibu maswali hayo, Waziri Mkullo alisimama na kusema alishajiandaa kujibu maswali yote kwa kuwa kabla ya kuja katika kikao hicho, alisoma vizuri na baada

ya kufika hotelini hapo alipewa mambo yote yaliyojiri kikaoni, hivyo ingekuwa rahisi kwake.

Hata hivyo, Waziri Mkullo alisema kwa kuwa wabunge wameamua awape majibu hayo kwa maandishi, atafanya hivyo na kuahidi kuwapa majibu hayo kabla ya kikao kijacho cha Bunge la Bajeti kinachotarajiwa kufanyika Juni.

Hata hivyo, Mkullo alijibu baadhi ya maswali aliyoyaita kuwa ni mepesi na kuwa alikuwa na majibu yake.

Pamoja na mambo mengine, wabunge hao walitaka kujua kwa nini bajeti ya serikali siku zote inakuwa tegemezi, kwa nini kunakuwa na utumiaji mbovu wa misamaha ya kodi na kutaka suala hilo liangaliwe upya.

Maswali mengine, ni kwanini pesa za bajeti zinazobaki kila mwaka katika baadhi ya wizara, hazionyeshwi katika bajeti ijayo kuwa zimetumikaje na zinaenda wapi.

Swali hilo liliulizwa na Mbunge wa Pangani, Mohamed Rished, kwanini ripoti ya CAG, haipelekwi moja kwa moja kwa Spika ambaye ndiye aliyemtuma kwa niaba ya wabunge na wananchi na badala yake, ripoti hiyo anakabidhiwa kwanza Rais ndipo ipelekwe bungeni na hatua zinazochukuliwa kwa halmashauri zinazopata hati chafu kwa kuwa, Ripoti ya CAG inaonyesha kila mwaka kuna halmashauri zinavurunda, lakini hazifanywi chochote.

No comments: