Thursday, May 29, 2008
Waziri Mkuu ashuhudia Upasuaji wa Moyo Muhimbili..
Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda (katikati) akishuhudia upasuaji wa moyo ulioongozwa na Daktari,William Mahalu wakati alipotembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
--------------
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda alishuhudia mgonjwa akifanyiwa upasuaji wa moyo (Kwa Kiingereza "open heart surgery") kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,ikiwa ni mwanzo wa mpango mkubwa wa kufanya operesheni za namna hiyo hapa nchini badala ya nje ya nchi.
Baada ya kushuhudia operesheni hiyo alikwenda wodini kuwakagua baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa moyo na wengine wanaojiandaa kufanyiwa.Tangu Mei 21, mwaka huu tayari wagonjwa watano wamekwishafanyiwa upasuaji huo uliokwenda salama, ukiashiria kuwa tiba ya aina hiyo inawezekana hapa nchini kwa kutumia wataalamu wa Kitanzania badala ya nje ya nchi, hasa India.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Prof. David Mwakyusa alimwambia Waziri Mkuu kuwa kwa miaka tisa tangu mwaka 1999 hadi mwaka jana, wagonjwa 586, ambao kati yao asilimia 70 ( wapatao 402) ni wa moyo, walipelekwa nje kwa upasuaji na kugharimu kiasi cha Sh. Bilioni 10.
"Tunatarajia tuondokane na gharama hizi kubwa kwa kufanya kazi hii ya upasuaji wa moyo hapa hapa Muhimbili," Profesa Mwakyusa alisema wakati akimwelezea Waziri Mkuu mpango huo. Kwa sasa shughuli hizo zinafanyika katika jengo la Taasisi ya Mifupa (MOI) eneo hilo hilo la Muhimbili, lakini jengio jipya la kitengo cha upasuaji wa moyo linatarajiwa kujengwa hapo hapo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mitambo, mashine na vifaa vya kazi hiyo vilipatikana kwa kughharimiwa na serikali. Wataalamu 27 wa Kitanzania, wakiwemo madaktari wa upasuaji, wataalamu wa ganzi, mafundi na wauguzi walipelekwa India kwa mafunzo ya mwaka mmoja hadi miwili ili kupata uzoefu wa tiba ya upasuaji wa moyo na wote wamekwisharudi nyumbani.
Waziri Mkuu Pinda alipongeza jitihada hizo na kusema kwamba serikali itaendelea kuziunga mkono ili kuleta ufanisi na kuhakikisha zinakuwa endelevu."Najua sasa wagonjwa watakuwa wengi na kazi itakuwa nzito. Lakini mjitume. Yale ambayo mtayaona hayaendi vizuri, msiyahamishie kwa wagonjwa bali tuleteeni sisi ili tupate njia za kuyatatua," alisema. Kuanza kwa mpango huo wa upasuaji wa moyo nchini kwa kutumia wataalamu wa hapa hapa ni mafanikio makubwa katika kutoa huduma za afya nchini na kutapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kwa tiba ya aina hiyo.
Imetolewa na:
Ofisi ya Waziri Mkuu,
S.L.P. 3021
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment