Wednesday, May 28, 2008
Wanaonituhumu Wananisingizia -Mkapa
RAIS Mstaafu wa awamu ya tatu, Mh Benjamin Mkapa (Pichani)amekanusha matumizi mabaya ya ofisi yake(ikulu) na kuanzisha biashara akiwa madarakani.Akihutubia wananchi katika Kijiji alichozaliwa cha Lupaso,Wilaya ya Masasi,Mkapa alisema wanaomtuhumu wanamchukia kwa kutowapendelea wakati wa utawala wake.
Katika hotuba yake hiyo aliyoitoa wakati wa kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya tiba kwa Kituo cha Afya kinachomilikiwa na Kanisa la Katoliki kijijini hapo, alisema; “Msisikilize uongo huo kwa sababu hauna msingi wowote isipokuwa ni chuki..hasa inayotokana na watu ambao walifikiri nitawapendelea … sikuwapendelea,wananisingizia” alisema Mkapa huku akishangiliwa na wanakijiji wenzake waliohudhuria makabidhiano hayo.
Alisema kuwa yeye si tajiri na kwamba tuhuma hizo ni za uongo na hivyo kuwataka wananchi kuzipuuza kwa kuwa hazina msingi wowote wala chembe ya ukweli.“Sina uwezo wa fedha ingawa najua mnasikia na kusoma mengi …naishi kwa pensheni yangu kutoka serikalini kutokana na kuwa kiongozi kwa miaka 10 ambayo hata Mzee Mwinyi anaishi hivyo maana sisi sote ni wastaafu.
Huo (uvumi) ni uongo …uongo ….uongo ….uongo …uongo….uongo….uongo,” alisema Mkapa.Katika hotuba yake hiyo Mkapa hakujibu tuhuma dhidi yake moja kwa moja Kwa kipindi kirefu sasa Mkapa amekuwa akituhumiwa kwa kuendesha biashara akiwa Ikulu na hasa kuhusu umiliki wa Kampuni ya Tanpower inayomiliki hisa nyingi katika Mgodi wa Makaa ya Mawe ya Kiwira mkoani Mbeya.
Imekuwa ikidaiwa kwamba Mkapa alishirikiana na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona katika kununua hisa za Kiwira kwa matarajio kwamba umeme ungezalishwa kutoka hapo baada ya muda mfupi ujao na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lingelazimika kuwalipa takribani Sh milioni 140 kwa siku, hata bila umeme kuzalishwa.Habari na Msimbe Lukwangule
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment