Mkoa wa Dar es Salaam, umewatahadharisha wananchi dhidi ya ulaji wa nyama ya `kitimoto` kutokana na kuibuka kwa homa ya nguruwe.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya Manispaa ya Ilala, Temeke na Kinondoni, ugonjwa huo hauna tiba wala chanjo.
Ilitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni homa kali, kushindwa kula, kuharisha na kutapika na kuvilia damu chini ya ngozi hususan sehemu za tumbo na miguu.
Ilitaja dalili zingine kuwa ni kupepesuka au kutetemeka, kupumua kwa shida, kutoa mapovu mdomoni, kukohoa na wakati mwingine kutoa machozi.
Taarifa hiyo ilisema kutokana na madhara na hasara kubwa za ugonjwa huo, halmashauri hizo zimepiga marufuku wafanyabiashara wa nguruwe kusafirisha ndani au nje ya Manispaa ya Ilala na Temeke nguruwe na mazao yake.
Mazao hayo ni nyama, mifupa, damu, soseji pamoja na mbolea.
``Hairuhisiwi kulisha nguruwe, mabaki ya nyama na mazao yake na hairuhusiwi kusafirisha nguruwe au mazao yake kutoka katika mashamba na maeneo yaliyoathirika na ugonjwa wa homa ya nguruwe bila kibali maalum kwa Daktari wa mifugo wa Manispaa husika,`` ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, ilisema wachinjaji wa nguruwe hawaruhusiwi kuchinja na kuuza nyama hiyo bila kibali cha Daktari wa mifugo wa manispaa husika.
Taarifa hiyo ilisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayepuuza maagizo hayo ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment