Saturday, May 31, 2008

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

--------------
Benki ya Dunia imeahidi kulisaidia bara la Afrika katika kutatua tatizo la chakula kwa kuongeza msaada katika mbolea na mbegu ili wakulima waweze kuongeza uzalishaji. "Tutawasaidia muweze kuondokana na tatizo la chakula, tunataka tuwasaidie katika matumizi ya mbolea na mbegu bora".


Alisema Rais wa Benki ya Dunia Robert Zoellick wakati wa mazungumzo na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ambaye pia ni Rais wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete walipokutana kwa ajili ya mazungumzo Mjini Yokohama leo mei 29,2008 mchana.Katika mazungumzo hayo Mhe. Zoellick amesema Benki ya Dunia imedhamiria kuongeza msaada na kubuni njia za kuongeza msaada katika kuendeleza kilimo na kuweza msaada huo kufikiwa kwa urahisi na nchi za Kiafrika ili kuondosha uhaba wa chakula.


Rais Kikwete ameishukuru Benki ya Dunia ambapo Rais Kikwete amemueleza Mheshimiwa Zoellick kuwa Tanzania inahitaji msaada zaidi katika kukuza uwezo wa wataalamu wa kilimo katika kufanya utafiti.


Rais Kikwete amemweleza Mhe. Zoellick kuwa kwa sasa Tanzania inafanya utafiti katika swala la kukuza na kuongeza ubora wa mbegu zinazohitajika katika mazingira ya Tanzania,lakini uwezo wa wataalamu hao bado ni mdogo hivyo kulifanya taifa kuagiza mbegu kutoka nje kwa asilimia 75,ilhali mbegu bora zinaweza kutengenezwa na kuzalishwa nchini.


Tukiweza kuongeza mbegu bora zinazozalishwa nchini kwetu mara dufu tutaondokana na tatizo kwa kiwango kikubwa"amesema Rais Kikwete.Mbali na uwezo wa kuzalisha mbegu bora, Rais amemueleza Mhe. Zoellick kuwa pamoja na serikali kutoa ruzuku kwenye mbolea ili kuongeza matumizi ya mbolea katika kilimo, hatua hiyo haionyeshi unafuu wowote kwa wakulima kwa vile bei ya mbolea duniani imepanda mara dufu.


"Msaada mkubwa unaoweza kutupa sisi Tanzania ni kutuongezea uwezo katika vituo vyetu vya utafiti wa mbegu na mbolea kwa ajili ya wakulima wetu kwani kilimo chetu kimedumaa kutokana na kuwa cha asili zaidi badala ya kuwa cha kisasa" Ameongeza.Mapema asubuhi Rais Kikwete ameongoza Kikao cha wakuu wa nchi na mashirika ya kimataifa katika mkutano uliojadili hali ya chakula na changamoto za bei za chakula duniani.


Katika kikao hicho Rais Kikwete amesema, wahisani wanajukukumu la kulisaidia bara la Afrika kutumia ardhi yake kwa ajili ya kilimo bora na cha kisasa ili kuongeza uzalishaji hasa kwa wakati huu ambapo kuna upungufu mkubwa wa chakula.Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Yasuo Fukuda amesema ifikapo mwezi Julai mwaka huu, Japan itakuwa imetenga $100milion za dharura za msaada wa chakula kwa Afrika.


Benki ya Dunia nayo imeahidi kuongeza pesa zaidi kutoka $4 billion za sasa hadi $6billion katika kilimo .Wakichangia katika kikao hicho wawakilishi mbalimbali kutoka Mfuko wa Chakula Duniani (WFP) amesema dunia inamhitaji mkulima wa Kiafrika sasa kuliko wakati wowote ule na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na serikali za Kiafrika ili kutatua tatizo hilo.


Nayo Benki ya Afrika ADB imesema inafanya marekebisho katika mfumo wake ili kuweza kutenga pesa zaidi katika kutatua swala la chakula barani Afrika.Rais pia amefanya mazungumzo na kukutana na viongozi mbalimbali kuzungumzia hali ya kisiasa na kidiplomasia ya nchi za Afrika,ambapo amefanya mazungumzo na Rais Omar Bashir wa Sudan na Louis Michel Kamishna wa Maswala ya kibinadamu na maendeleo katika Umoja wa Ulaya,ambapo amemweleza kuwa Umoja wa Afrika na nchi za SADC zitapeleka waangalizi katika marudio ya uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao.


Rais Kikwete yuko nchini Japan kuhudhuria mkutano kuhusu maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development (TICAD IV) unaomalizika kesho (30 Mei 08); ameshiriki katika vikao mbalimbali na kuongoza baadhi ya mikutano ambapo atashiriki katika kupitisha azimio la Yokohama na baadaye,yeye na Waziri Mkuu wa Japan Mheshimiwa Fukuda, watafanya mkutano na waandishi wa habari na kuondoka mara baada ya mkutano huo.Rais na ujumbe wake watawasili Dar-es-Salaam Tarehe 31 Mei,08.
Mwisho
Imetolewa na Premi Kibanga
Yokohama,
Japan29 Mei, 08

No comments: