Saturday, May 31, 2008

Japan yamwaga Bilioni 21.3 Kuboresha Umeme jijini .....


Pichani ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi,Gray Mgonja
------------
SERIKALI ya Japan imeisadia Tanzania sh bilioni 21.3 kwa ajili ya mradi wa uboreshaji na upanuaji wa miundombinu ya usambazaji wa huduma ya umeme katika Jiji Dar es Salaam.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya kufanyika kwa makubaliano na utiaji saini wa mradi huo, kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja na Balozi wa Japan nchini, Makoto Ito, wakati wa hafla fupi iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia kuhusu mradi huo, Balozi Ito alisema umebuniwa kwa sababu upatikanaji wa uhakika wa nishati ya umeme utasaidia kuondoa umasikini na kukuza uchumi.
Alisema Dar es Salaam ni kitovu cha biashara, hivyo jiji linahitaji umeme wa uhakika wakati wote.

“Msaada huo umetolewa ili kuweza kutatua tatizo la umeme katika Jiji la Dar es Salaam na kukipunguzia mzigo kituo kidogo cha huduma ya umeme cha Ilala,” alisema Balozi Ito.
Alisema fedha hizo zitatumika kuboresha kituo kidogo cha Ubungo na ujengaji wa kituo kingine kama hicho katika eneo la Oysterbay. Ito aliongeza kuwa msaada huo utakuwa ni wa awamu tatu, ambapo awamu ya kwanza inaanza mwaka huu, ya pili itatekelezwa mwaka ujao na ya tatu 2010.

Kwa upande wake, Mgonja aliishukuru Japan kwa kuendelea kutoa msaada na kuongeza kuwa fedha hizo ni nyongeza ya msaada wa kwanza wa kuisaidia Tanzania kuboresha huduma hiyo nchini. Alisema msaada huo utasaidia kuboresha huduma za umeme katika maeneo ya Mikocheni, Oysterbay, Msasani, Magomeni, katikati ya jiji, Kariakoo na Kurasini. Habari hii na kutoka ukumbi wa habari Maelezo

No comments: