Taarifa kwa Vyombo Vya Habari
May 23 2008
'Sanaa imeokoa maisha yangu' asema msanii anayeunda zawadi za shindano la Faidika na BBC
Msanii kutoka Uganda, mshindi wa tuzo kadhaa, Peter Oloya, amechaguliwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, kubuni na kuunda tuzo za washindi wa shindano la vijana. Faidika na BBC linatafuta kijana mwenye umri wa kati ya miaka 16 hadi 24, ambaye ana wazo zuri la biashara, ambalo litakuwa na manufaa kwa jamii. Zawadi ya kwanza ina thamani ya Dola Elfu Tano za Marekani.
Peter ataunda mataji ambayo yatazawadiwa kwa washindi wa kitaifa nchini Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda, na pia katika fainali itakayofanyika Kampala, mwezi Juni. Peter aliwasilisha michoro yake kupitia Ruwenzori Sculpture Foundation, ambayo inaratibu ubadilishanaji wa utamaduni na elimu kati ya wasanii wa Afrika na Uingereza. ' Nimefurahishwa na BBC Idhaa ya Ulimwengu, shirika ambalo naliheshimu kwa ubora wa kazi yake, kwa kunichagua mimi katika nafasi kubwa kama hii katika shindano hili. Ni ndoto ambayo kwangu imekuwa kweli'
'Usanii ndio maisha yangu, na hakika imejenga mwelekeo wa maisha yangu' ameongeza msanii huyo mwenye umri wa miaka 30. 'nimepitia maisha ya vita na kushuhudia mengi wakati nikiwa mdogo, na nikatumia sanaa yangu kama njia ya kuondokana na nyakati hizo ngumu, kwa hakika fani hii inaendelea kunisaidia kila siku' ameongeza Peter.
Changamoto kubwa kwa Peter ilikuwa kubuni kitu ambacho kinatoa taswira nzito. ' Niliambiwa na BBC kubuni kitu kinachoonesha mtazamo wa mbali na uvumbuzi unaoakisi kufanya vyema katika biashara, na vilevile kuonesha kustawi na kukua kwa jambo. Ilikuwa kazi ngumu, lakini nimeweza kupata suluhu ya hilo'
Suluhu hiyo, ni sanamu ya mtu aliyesimama katika ramani ya nchi zinazoshiriki katika shindano hili, za Afrika Mashariki na Kati na zinazozungumza kiswahili. Mfano huyo wa mtu amesimama akitazama anga huku akiwa amenyoosha mikono yake, inayoshikilia nyota. Peter anaeleza kuwa mchongo huo 'Unakutaka unyooshe mikono yako kufikia nyota, maana yake uendelee kukua, na uelewe ya kwamba hakuna linaloshindikana. Shaba na kioo ambazo zimetumika kutengeneza tuzo hiyo zinashabihiana na zitadumu kwa miaka mingi'
Peter, ambaye alizaliwa katika kijiji cha Lemo Bongolewich katika wilaya ya Kitgum, Kaskazini mwa Uganda, anasema anaweza kujihusisha na vijana wanaoshiriki katika shindano la Faidika na BBC. Akiwa ni msanii aliyejifundisha uchoraji, na ambaye alifanya jitihada na kujilipia mwenyewe elimu ya Sekondari hadi chuo kikuu, anasema ' Mafanikio sio jambo la kupatikana kwa bahati, bali kupitia dhamira na kazi ngumu, mambo ambayo natazamia washiriki wa shindano hili watakuwa nayo. Kuenzi jamii pia ni muhimu, na ni jambo ambalo limenivutia katika shindano la Faidika na BBC.
Peter amekuwa akisaidia jamii yake kupitia shirika lijulikanalo kama Sanaa kwa maendeleo ya jamii, ambalo alilianzisha mwaka 2004. Likiwa na makao yake katika wilaya za Kitgum na Gulu, Kaskazini mwa Uganda, shirika hilo linatoa huduma za elimu ya sanaa na uchongaji, na pia elimu ya uraia kupitia sanaa ya maigizo kwa vijana wa eneo hilo. Sehemu ya shirika hilo linadhaminiwa na fedha zinazotokana na mauzo ya kazi zake Peter. 'Watoto wengi na vijana wanaokuja kujiunga nasi wanakuwa wameathiriwa na vita, lakini mafunzo tunayotoa yanawasaidia kuondokana na hali waliyonayo. Kusaidia kuleta hali ya kawaida kwa vijana ni muhimu kwangu, kwa kuwa wao ndio mategemeo ya baadaye, na siku moja watasaidia kuleta amani nchini'
Peter, ambaye anasema kazi yake imechochewa na msanii wa Kiingereza Damien Hirst, ametunukiwa zawadi kadhaa kwa kazi zake za uchongaji, ikiwemo zawadi ya kwanza ya shindano la ' Sanaa kwa amani' la Uganda, na zawadi nyingine ya uchongaji kutumia shaba, lililoendeshwa na shirika la Uingereza la uchongaji, Pangolin Editions, katika chuo kikuu cha Makerere.
Peter alifuzu katika fani ya uchongaji katika kitivo cha uchoraji cha Margaret, kilichopo chini ya Makerere, na kupata shahada ya uchoraji sanifu. Amefanya kazi nyingi katika sanaa hiyo ikiwemo kuchonga zawadi aliyotunukiwa Malkia wa Uingereza, Elizabeth wa pili, wakati wa mkutano wa wakuu wa mataifa ya Jumuiya ya Madola, mjini Kampala, mwaka 2007. Mapema mwaka huu, Peter aliwasilisha picha ya kuchora kutumia rangi za mafuta, kwa rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, alipozuru chuo kikuu cha Makerere.
Picha ya Peter Oloya inaweza kupatikana iwapo inahitajika.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana na:
Christine George, Afisa mwenezi msaidizi, BBC World Service
+44 (0) 2075571142; christine.george@bbc.co.uk
Maelezo kwa Wahariri.
Muda wa kupokea michanganuo ya shindano la Faidika na BBC, sasa umekwisha. Taarifa zaidi kuhusu shindano zinapatikana katika mtandao wetu bbcswahili.com/faidika
BBC Idhaa ya Kiswahili ni Shirika la Utangazaji ambalo hutoa huduma zake kupitia radio na kwenye mtandao kwa wasikilizaji wanaozungumza Kiswahili barani Afrika na ulimwengu mzima kwa ujumla. Kipindi cha BBC cha asubuhi Amka na BBC hurushwa hewani saa 12.00 asubuhi saa za Afrika mashariki, na hukuletea habari za eneo zima na duniani, pamoja na muziki na habari mbalimbali za kijamii. Kipindi maarufu cha BBC cha habari na uchambuzi Dira ya Dunia huanza saa 12 na nusu jioni. Leo Afrika husikika saa tatu kasorobo Afrika Mashariki, na hukuletea habari mbalimbali zilizotokea barani Afrika kwa siku hiyo. Mtandao wa BBC kwa kiswahili unapatikana katika bbcswahili.com. Katika mtandao huu, unaweza kupata taarifa za maandishi, matangazo yetu, makala na uchambuzi wa habari za Afrika na dunia nzima. Pia katika mtandao huu utapata taarifa na matangazo ya kipindi maarufu cha Kimasomaso, ambacho hutoa elimu ya afya ya uzazi na kuchambua mila na desturi zinazozingira suala zima la uzazi. Kipindi hicho kilianzishwa na kitengo cha kimataifa cha BBC cha misaada - BBC World Service Trust.
BBC World Service - Idhaa ya Dunia, ni shirika la habari la kimataifa la utangazaji linalotoa huduma za matangazo kwa lugha 33 mbalimbali. Shirika hili linatumia njia kadhaa kuwafikia wasikilizaji wake milioni 183 ulimwenguni kote, kwa kupitia Masafa mafupi, masafa ya kati, FM, satellite na viunganishi. Vituo washirika vya radio vipatavyo 2,000 hupitisha matangazo ya BBC, huku vituo kadhaa vukirusha taarifa zake kupitia simu za mkononi na vifaa mbalimbali visivyotumia nyaya. Wavuti wa BBC unatoa habari mbalimbali kwa maandishi, sauti na video, na vilevile kutoa nafasi kwa wasikilizaji kushiriki moja kwa moja katika vipindi kufuatana na matukio ya duniani. Takriban watu milioni 700 huvinjari katika wavuti huu kwa mwezi, na hivyo kuvutia karibu watumiaji milioni 40 kwa mwezi. Kwa taarifa zaidi tembelea bbcworldservice.com. kufahamu zaidi kuhusu Idhaa ya Kiingereza ya BBC, au kujiandikisha kupata majarida ya kwenye mtandao tembelea bbcworldservice.com/schedules.
No comments:
Post a Comment