Wednesday, May 28, 2008

Mkapa achokoza nyuki

Mkapa achokoza nyuki

Na Muhibu Said

WATU wa kada mbalimbali jijini Dar es Salaam jana waligeuka kama nyuki waliochokozwa baada ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kujaribu kujisafisha tuhuma zinazomkabili, huku wengi wakiwa hawaridhiki na utetezi wake na kumtaka ajibu tuhuma za ufisadi zinazomkabili moja baada ya nyingine.

Watu hao, wakiwamo wanasiasa, wabunge na wanasheria, kwa nyakati tofauti, pia wamemtaka Mkapa kutokwenda kujisafisha kijijini, badala yake azungumze na waandishi wa habari ili apate kuulizwa maswali na kuzitolea ufafanuzi tuhuma za ufisadi zinazomkabili.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema Mkapa hapaswi kwenda kuwaeleza wanakijiji kuhusu ufisadi anaotuhumiwa kuufanya wakati wa utawala wake, kwani hawawezi kumhoji, badala yake wataishia kumpigia makofi kwa vile aliwapelekea msaada wa vifaa vya zahanati.

Alisema anachotakiwa kufanya ni kuzungumza na waandishi wa habari ili ajibu tuhuma hizo kwa vile zina vielelezo na Watanzania waweze kumwelewa.

"Hizi ni tuhuma nzito, alipaswa kuzijibu akizungumza na waandishi wa habari. Na badala ya kuzieleza kwamba ni uongo, tuhuma hizi zimetolewa na vielelezo. Na ni nyingi," alisisitiza Profesa Lipumba.

Alisema tuhuma ya kwanza nzito, ambayo Mkapa anapaswa kuijibu, ni ile inayohusu kuanzisha kampuni ANBEN mwaka 1999 ambapo anadaiwa kuwa alikopa dola nusu milioni kutoka benki wakati huo akiwa rais na akiwa Ikulu na akaweza kuzirejesha katika kipindi cha mwaka mmoja.

Lipumba alisema kitendo cha mtu kuanzisha kampuni akiwa kama rais, ni ukiukwaji wa maadili ya uongozi, kwani kwa kawaida viongozi hata wakiwa na makampuni, huwa wanamweka mtu mwingine anayeendesha kusudi pasiwe na migongano ya masilahi.

"Hilo hajalijibu. Kwamba, ilikuwaje akaanzisha kampuni mwaka 1999 na akakopa nusu milioni na akawa mfanyabiashara bora kweli kuweza kuzirudisha fedha hizo katika kipindi cha mwaka mmoja. Si rahisi kukopa dola nusu milioni ambazo ni zaidi ya Sh milioni 500 na kuweza kuzirejesha na kulipa riba kwenye benki. Hilo la kwanza," alisema Lipumba.

Lipumba alisema shutuma nyingine nzito ambazo Mkapa anatakiwa azijibu ni zile zinazohusiana na rada ambazo zimethibitishwa na Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza ambayo imekuwa ikifanya uchunguzi dhidi ya Kampuni ya BAE System iliyoiuzia Tanzania rada hiyo mwaka 2002.

Alisema mwaka 1995, kulikuwa na jaribio la kuiuza rada hiyo na kwamba, ili serikali iinunue, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitakiwa iweke dhahabu iliyonayo kama dhamana ya kununulia ili kama serikali itashindwa kulipa, dhahabu hiyo iende kwa muuzaji.

Lipumba alisema jaribio hilo lilikakataliwa na mradi huo wa kununua rada ukafa, lakini ulikuja kufufuliwa baada ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kufariki dunia.

Alisema pamoja na mradi huo kufufuliwa, SFO imeeleza kwamba, wakala Shailesh Vithlani aliyesimamia ununuzi wa rada hiyo, amelipwa rushwa ya dola 12 milioni na Kampuni ya BAE, zikawekwa kwenye akaunti nchini Uswisi.

"Mimi binafsi nilikuwa nikipiga kelele kwamba, hii rada ina kila harufu ya rushwa. Serikali ikapinga, ikasema ni utaratibu mzuri kabisa, hauna matatizo. Leo hii tunafahamishwa kwamba, kulikuwa na rushwa ya dola milioni 12," alisema Lipumba.

Alisema wakati ununuzi wa rada hiyo unafanyika, ripoti ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Mambo ya Anga (ICAO) ilitoa taarifa kwamba, rada ambayo inakidhi mahitaji ya Tanzania inaweza kupatikana kwa dola 5 milioni, lakini serikali ya Tanzania ikaenda kununua rada ya dola 40 milioni, huku wakala aliyesimamia ununuzi huo, akiwekewa dola 12 milioni.

Alisema wakala huyo ndiye ambaye alikuwa wakala wa kununua ndege ya rais iliyogharimu zaidi ya dola 40 milioni ambayo pia yeye (Lipumba) aliipigia kelele kwamba haihitajiki, kwa vile ni gharama kubwa, lakini Mkapa wakati huo akasema kwamba, ni muhimu.

Alisema wakala huyo pia alishiriki katika ununuzi wa magari na helikopta za jeshi na kwamba, mambo yote hayo yalitokea katika kipindi cha Mkapa, licha ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Maendeleo, Claire Short wa Uingereza kupinga katika Bunge la nchi hiyo kwamba, rada hiyo isinunuliwe na serikali ya Tanzania kwa vile ina kila harufu ya rushwa, ingawa akazidiwa nguvu na Waziri Mkuu wake, Tony Blair.

"Kwa hiyo kuna suala la rada anapaswa atujulishe, imekuwaje wakati sisi tulikuwa tunamweleza kwamba, ununuzi wa rada, una kila harufu ya rushwa na sasa imethibitishwa kwamba, Shailesh Vithlani alilipwa dola 12 milioni. Je, yeye alipatiwa chochote katika hili? Swali hilo atujibu," alisema Lipumba.

Alisema tuhuma nyingine, inahusu suala la ununuzi wa mgodi wa Makaa ya Kiwira ambapo taarifa zinaeleza kwamba, Mkapa na jamaa zake wa familia pamoja na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Yona walianzisha kampuni ya TanPower Resources Limited iliyonunua mgodi huo kwa bei poa ya Sh milioni 700, lakini wamelipa Sh milioni 70.

Alisema kutokana na hali hiyo, Mbunge wa Vunjo (CCM), Aloyce Kimaro alilieleza suala hilo Bungeni.

"Sasa Mheshimiwa Aloyce Kimaro ana chuki gani binafsi dhidi ya Mkapa, ama Mheshimiwa Mkapa alimnyima nini Kimaro, mpaka sasa Kimaro amelieleza hili na kwamba, katika mkataba huu kuna Capital Payment ambapo kila siku tunalipa Sh milioni 146 kama Capital Charge. Hilo anapaswa kulieleza," alisema Lipumba.

Alisema kashfa nyingine, ni ufisadi wa Sh 133 bilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje katika BoT ambazo alisema benki hiyo isingeweza kutoa malipo kwenye makampuni husika 130 bila serikali kuwa na taarifa.

"Pana kashfa nyingine ambazo bado hazijafanyiwa uchunguzi, kama gharama za majengo ya ofisi za BoT", alisema.

Alisema Mkapa alipoanza kutawala, alitangaza mali zake, lakini alipoondoka madarakani hadi sasa hajasema ameondoka akiwa na mali kiasi gani.

"Laiti Mwalimu angelikuwa hai baada ya shutuma zote hizi, nadhani angejilaumu sana kwamba amedanganywa vibaya na mwanafunzi wake aliyemsimamia na kumpigia debe mpaka kuwa rais," alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa alisema yeye ni kati ya waliomtuhumu Mkapa hadharani kwa rekodi na kwa hiyo hajawahi na kamwe hatoajiriwa na serikali.

Hivyo, Dk Slaa ambaye pia ni Mbunge wa Karatu alisema anachotakiwa kukifanya Mkapa ni kujibu tuhuma za ufisadi zinazomkabili na kwamba, hawatahitaji kusikia kutoka kwake jambo la pensheni ambalo hajaulizwa.

"Brela (Kitengo cha serikali cha Kusajili Makampuni) inaonyesha yeye (Mkapa) na mkewe, walianzisha kampuni yenye S.L.P 15 Luthuli Street akiwa Ikulu. Kwa maana alikuwa mjasiriamali akiwa Ikulu. Tunataka kujua mtu huyo ni yeye au la. Na pia alilipa pango ya jengo la Ikulu shilingi ngapi kwa kuitumia Ikulu kufanya biashara?" alisema Dk Slaa.

Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro alimtaka Mkapa kujibu hoja na kwamba, maelezo aliyoyatoa Bungeni kuhusu Mkapa namna alivyonunua mgodi wa Kiwira bila kufuata utaratibu, alifanya hivyo kwa vile zama hizi ni za ukweli na uwazi.

"Hajajibu hoja. Wabunge wangetaka kusikia hayo yanayosemwa dhidi yake. Tunataka yasiendelee kutokea, pia serikali ibadilike, bunge libadilike na viongozi wa ngazi zote wabadilike, watumikie wananchi, siyo wananchi wawatumikie," alisema Kimaro.

Kimaro alisema ataendelea kusema ukweli kwani fitina kwake ni mwiko na Mkapa ndiye muasisi wa kauli mbiu ya uwazi na ukweli.

Naye Hussein Issa anaripoti kuwa, Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Cyriaws Kamugisha, alisema iwapo Mkapa atapatikana na hatia ya kuhusika na tuhuma za ufisadi, anatakiwa afikishwe kizimbani kwani, sheria ni msumeno.

Alisema ikiwa rais aliyeko madarakani akiwa na kosa la madai, anatakiwa ashitakiwe na kuhoji iweje aliyemaliza muda wake asishitakiwe ikiwa ana kosa la kujibu?

Tuhuma za kununua Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira (KMCL) ulioko wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya , zililipuka mwanzoni mwa mwaka huu.

Kufuatia tuhuma hizo, hadhi ya Mkapa ambaye aliingia madarakani akiwa safi na kujulikana 'Mr Clean' inazidi kuporomoka miongoni wananchi mbalimbali, ambao wanaamini kuwa alitumia vibaya wadhifa wake kujipatia mali kinyume na maadili ya uongozi.

Juzi Mkapa alikaririwa na vyombo vya habari, akisema watu wanaomtuhumu wamefanya hivyo kwa vile aliwanyima vyeo wakati alipokuwa madarakani kwa miaka 10 na kwamba watu wote wanaomuita fisadi ni wa kupuuzwa kwa kuwa wana chuki binafsi naye.

Mkapa alikuwa akiwahutubia wanakijiji wa Lupaso wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, baada ya kukabidhi msaada wa vifaa vya tiba kwa uongozi wa kituo cha afya kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki kijijini hapo.

No comments: