Na Theodatus Muchunguzi (Mwananchi)
RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa sasa anatuhumiwa kwa ufisadi kutokana na alivyotumia Ikulu kinyume na maadili ya uongozi kufanya biashara zake binafsi pamoja na kujiuzia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira mkoani Mbeya.
Tuhuma hizo zilianza siku nyingi, lakini zimepamba moto katika siku za karibuni, ambapo limeibuka shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi wanaolalamikia na kuchukizwa na ufisadi unaofanywa na viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza nchi kujitajirisha na kuwaacha Watanzania wengi wakibaki katika umaskini mkubwa.
Wakati tuhuma dhidi ya Mkapa zinaanza kutolewa, baadhi ya wananchi walidhani kuwa kiongozi huyo mstaafu alikuwa anapakwa matope na maadui zake wa kisiasa, lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo wananchi wengi walivyoanza kuamini kuwa tuhuma hizo zina ukweli ndani yake.
Kinachowasukuma wananchi kukasilishwa na tuhuma hizo na kuamini kuwa Mkapa anahusika ni kitendo chake cha kuamua kukaa kimya badala ya kujitokeza na kueleza umma ukweli kuhusiana na tuhuma hizo.
Kuna wakati vyombo vya habari vilimuuliza Mkapa atoe ufafanuzi wa tuhuma hizo, lakini aliishia tu kusema kuwa hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa amestaafu siasa. Kauli yake ilionekana kuwa ya kiburi, dharau na yenye lengo la kukwepa tuhuma hizo. Ninasema ililenga kukwepa ukweli kwa sababu siyo kweli kuwa Mkapa amestaafu siasa.
Kimsingi, Mkapa bado ni mwanasiasa hasa na bado anashiriki kwa kiwango kikubwa katika utoaji wa maamuzi nyeti na makubwa yanayohusu mustakabali wa nchi hii na watu wake. Pamoja na kustaafu urais, yeye ni mjumbe wa kudumu wa vikao vya Chama cha Mapinduzi (CCM), vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu (CC); Chama ambacho kinatawala na kinaunda serikali.
Hivyo anaposimama na kudai kuwa amestaafu siasa ni uongo na anafanya hivyo kwa kukwepa kuwajibika na mambo mabaya aliyoyafanya wakati akiwa madarakani.
Kwa ujumla, hakuna binadamu yeyote ambaye anaweza kudai kuwa si mwanasiasa kwa kuzingatia kuwa maisha ya kila siku ya mwanadamu yanatawaliwa na siasa kama mwanafalsafa wa Ugiriki Aristotle alivyosema kuwa �human being is a political animal�.
Kingine kinachomfanya Mkapa akadhani kuwa hawezi kuchukuliwa hatua kwa mambo mabaya aliyotenda akiwa madarakani ni kinga inayotolewa na katiba ya nchi. Lakini mimi nadhani kuwa kinga hiyo inatumika vibaya kwa sababu inapaswa kumlinda rais kutokana na mambo aliyoyafanyia uamuzi akiwa na kofia ya urais na si mambo yake binafsi, la sivyo hatuna budi kubadili kifungu hicho ili kila mtu awe chini ya sheria.
Suala la Mkapa na mkewe, Anna, kusajili kampuni binafsi ya Anbem Limited mwaka 1999 ikiwa ni miaka minne tu baada ya kuingia madarakani ni suala binafsi, ambalo Mkapa anapaswa kuchukuliwa hatua kwa maana ya kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua zozote za kisheria ikiwa itabainika kuwa aliitumia kampuni hiyo vibaya, au kutumia madaraka yake kupinda sheria na taratibu katika mchakato mzima wa kununua mgodi wa Kiwira.
Tuhuma dhidi ya Mkapa zinasikitisha na kushangaza Watanzania wengi, ambao waliamini kabisa kwamba alikuwa na uadilifu wa hali ya juu kabla ya kuteuliwa na CCM kuwa mgombea wake wa urais mwaka 1995. Wengi walimchukulia Mkapa kuwa alikuwa mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Mwalimu Nyerere kwa kuamini kuwa Mkapa ndiye mtu mwadilifu na ambaye alistahili kuwa kiongozi wa nchi hii kupambana na rushwa iliyoonekana kuitafuna nchi, aliamua kubeba msalaba mkubwa wa kumnadi kwa wananchi katika baadhi ya mikoa nchini.
Mwalimu Nyerere alifikia mahali akaandika kitabu cha �Viongozi wetu na hatima ya Tanzania�. Katika kitabu hicho, aliukosoa uongozi wa awamu ya pili kuhusu namna ulivyokuwa unashughulikia masuala nyeti ya nchi hasa suala la Muungano.
Aliwataja wazi wazi baadhi ya viongozi hasa John Samwel Malecela, aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais pamoja na Horace Kolimba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM kwa kumshauri vibaya Rais Ali Hassan Mwinyi na kusema hawafai kuwa viongozi.
Mwalimu alikiandika kitabu hicho wakati uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ukikaribia. Alikuwa anajua kuwa Malecela na Kolimba wangechukua fomu za kuomba uteuzi wa CCM kuwania urais na alijua fika kuwa Malecela alikuwa anaungwa mkono sana ndani ya chama hicho, kiasi kwamba Mkapa asingeweza kufua dafu.
Kauli za Nyerere katika vikao vya NEC na CC kabla ya uteuzi wa mgombea urais wa CCM zilibainisha wazi wazi kuwa mgombea aliyemtaka ni Mkapa kwa kigezo cha kutokuwa na kashfa yoyote ya rushwa.
Nilishuhudia Nyerere akizomewa na kurushiwa mawe katika miji ya Moshi, Morogoro na Iringa wakati akiwaambia wananchi kuwa Mkapa ndiye aliyekuwa ana sifa za kuwa rais kuliko wagombea wote ndani ya CCM na upinzani.
Nakumbuka wakati tunaingia uwanja wa ndege mjini Moshi nikiwa katika timu ya waandishi wa habari waliofuatana na Nyerere katika miji ya Moshi, Morogoro, Iringa na Songea, tulipata wakati ngumu wa kuzomewa na wananchi waliokuwa wanampinga Nyerere kumkampenia Mkapa.
Siku hiyo hiyo jioni katika uwanja wa Mashujaa mjini Moshi, mkutano wa Nyerere ulimalizika huku watu wakimzomea na kutaka kumrushia mawe wakati anasisitiza kuwa Mkapa ndiye mtu safi.
Akihutubia mkutano wa hadhara siku iliyofuatia katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro, Mwalimu Nyerere alisema Tanzania ina watu wawili wasafi na wenye uwezo wa kuongoza nchi na kuwataja kuwa ni Mkapa na Dk Salim Ahmed Salim.
Katikati ya wiki nilishangaa kusikia watu wazima watatu katika sherehe ya mkesha wa kumuaga bibi harusi jijini Dar es Salaam wakiwa wameketi meza moja, wakizungumzia tuhuma za ufisadi zinazomkabili Mkapa.
Nilijaribu kuwasikiliza nikagundua kuwa zimewagusa na kuwakasirisha Watanzania wengi. Mmoja wao alisema kuwa inashangaza kuona Mkapa akikaa kimya huku akikabiliwa na tuhuma hizo.
Mwingine akasema kuwa ni aibu kwa Mkapa, ambaye nchi hii ilimchukulia kuwa ni mtu safi na mtoto wa Nyerere. Mtu huyo aliongeza kuwa Mkapa aliaminika kuwa ni mtu safi kiasi cha kupewa jukumu la kufuatana na Papa John Paul ll katika maeneo mbalimbali wakati wa ziara yake nchini mwaka 1990.
Tuhuma dhidi ya Mkapa pia zinamtia doa Rais Kikwete na serikali yake kwa kuwa mawaziri kadhaa waliokuwa katika serikali ya Mkapa na kurejeshwa katika serikali ya sasa wanatuhumiwa kwa ufisadi pamoja na Mkapa mwenyewe. Rais Kikwete awali alisema serikali haina mpango wa kumchukulia hatua Mkapa na kuwataka wananchi wamuache Mkapa apumzike.
Baada ya tuhuma dhidi ya Mkapa kutolewa na watu wengi wakiwemo wabunge, hatimaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema serikali itazichunguza tuhuma dhidi ya viongozi wastaafu waliotenda kinyume cha maadili.
Ingawa Pinda hakumtaja moja kwa moja Mkapa, lakini bila shaka alikuwa anawagusia wastaafu wakiwemo Mkapa na aliyekuwa waziri wake wa Nishati na Madini, ambaye alishirikiana naye katika kujimilikisha mgodi wa Kiwira kwa bei ya kutupa Sh 700 milioni tofauti na thamani halisi ya Sh 4 bilioni na bila kutoa ushindani kwa watu na kampuni zingine.
Sijui kama Pinda alitoa kauli hiyo bungeni kwa nia ya dhati kutokana na kutoa kauli hiyo wakati akijibu swali la papo kwa hapo na mbunge wa CUF, Hamad Rashid Mohamed. Nina wasi wasi na uchunguzi wa serikali, ambao ni dhahiri utahusisha taasisi kama Takukuru, ambayo mwenendo wake wa utendaji unatiliwa mashaka na wananchi wengi hasa baada ya kutoa ripoti iliyoficha ukweli kuhusu kampuni hewa ya Richmond.
Haya ya Mkapa yananishawishi nikubaliane na Mwanafalsafa mwingine wa Ugiriki, Plato aliyesema viongozi wa dola wasimiliki mali wala familia. Huyu alijua kuwa kama watamiliki mali watataka kujilimbikizia, na kuzipendelea familia zao kama inavyojionyesha katika sakata hili.
Hatua inayoweza kuchukuliwa katika kubainisha ukweli kuhusu tuhuma za ufisadi zinazomkabili Rais mstaafu Mkapa ni kwa kuundwa Kamati Teule ya Bunge ambayo itafanya uchunguzi wake kwa uhuru na kuwasilisha matokeo ya uchunguzi huo bungeni.
Uchunguzi wa Kamati Teule ya Bunge siyio rahisi kuficha ukweli na una nguvu za kisheria na za kimahakama hivyo unaweza kubainisha ukweli huo bila kumwogopa mhusika. Funzo tulilolipata kutokana na Kamati ya Dk Harrison Mwakyembe katika kuchunguza kashfa ya Richmond linatufanya tuliamini Bunge kuliko taasisi zingine.
Baurapepe:theodatusm@yahoo.com Simu: 0737038475
No comments:
Post a Comment