Thursday, May 15, 2008
Natishiwa kuuwawa-Magufuli..
WAZIRI wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Bw. John Magufuli Pichani,amesema ametumiwa ujumbe wa kutishia maisha yake kwa njia ya simu ya mkononi kutokana na utendaji wake katika wadhifa alio nao.
Alisema hayo wakati akihutubia wananchi katika sherehe ya uzinduzi wa kiwanda cha kusindika minofu ya samaki cha National Investiment Company Limited (NICOL) kilichoko maeneo ya Ilemela .
Alisema ujumbe huo wa kutishia maisha yake unatokana na yeye kusimamia uchomaji makokoro yapatayo 700 kazi iliyoshuhudiwa na baadhi ya maofisa wa Wizara yake kutoka Dar es Salaam wakiwamo wa hapa na viongozi mbali mbali wa ngazi ya mkoa na wananchi. Uchomaji makokoro hayo ulifanyika katika dampo ya Buhongwa katika kata ya Buhongwa.
Akihutubia wananchi katika sherehe hiyo, Bw. Magufuli alisema ametumiwa ujumbe mara nyingi kuwa akiendelea kuchoma makokoro ya wananchi, maisha yake yatakuwa hatarini. Aidha, alisema kutokana na vitisho hivyo, ataendelea na kazi aliyopewa na Watanzania katika kusimamia rasilimali ya nchi wakiwamo viumbe ndani ya Ziwa Victoria.
Aliwataka viongozi wa ngazi zote kuanzia kata hadi mikoa, kusimama kidete katika kupiga vita uvuvi haramu katika Ziwa Victoria, ambapo hadi sasa kutokana na utafiti uliopo, unaonesha samaki aina ya sangara ambao huliletea Taifa kipato kikubwa, wanaelekea kutoweka. Alisema si mara yake ya kwanza kupokea vitisho kama hivyo kupitia simu ya mkononi na kuongeza kuwa hata wakati akiwa Waziri wa Ardhi, alipokea vitisho kama hivyo.
Bw. Magufuli aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni kuongoza wizara hiyo baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri wakati akiwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Waziri huyo alionesha uwezo wake wa kuchapa kazi wakati akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi katika awamu ya tau iliyongozwa na Rais Benjamin Mkapa, hata kupandishwa na kuwa Waziri Kamili na kuitumikia awamu hiyo hadi mwaka 2005.
Kote huko Bw. Magufuli alifanya kazi kwa moyo wa kujituma bila kuogopa vitisho na kujijengea sifa kubwa iliyosababisha baadhi ya watu kupendekeza agombee urais mwaka 2005, lakini hakuwa tayari. Mbali na hiyo, baadhi ya wananchi waliotambua mchango wake katika nafasi mbali mbali alizopewa kusimamia, walikuwa wakipendekeza ateuliwe kushika nafasi ya juu ikiwa ni pamoja na uwaziri mkuu.
Picha:Bob Sankofa
Habari:George Boniphace
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment