Saturday, May 10, 2008

Akutwa na Fuvu la Mtu..


Kamanda wa Polisi mkoani Arusha,Bw. Basilio Matei akionyesha fuvu la kichwa cha binadamu na tunguli alivyokutwa navyo mganga wa kienyeji,Bw. Juma Bakari maarufu kama 'Kimbunga' mjini humo jana.Picha na Magesa Magesa.
---------------
JESHI la Polisi mkoani hapa limamshikilia mganga mmoja wa kienyeji kwa tuhuma za kukutwa na fuvu la kichwa cha binadamu na rundo la matunguli.Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Bw. Basilio Matei ,alisema mtu huyo alikamatwa juzi saa moja jioni katika Kijiji cha Engutoto.
Alimtaja mtu hiyo kuwa ni Bw.Juma Bakari, maarufu kama 'Kimbunga' na alisema kuwa kukamatwa kwa mganga huyo kunafuatia wananchi wa eneo hilo kutoa taarifa polisi baada ya kumuona akiwa na fuvu hilo. Kamanda Matei, alisema hata hivyo maelezo yake ni kama sinema kwani alipotakiwa kueleza wapi alipopata fuvu hilo alidai alilitoa tumboni mwa mnyama ajulikanaye kama Karunguyeye.
Alisema mtu huyo alidai kuwa Mei 4 mwaka huu wakati akiwa dukani kununua mafuta ya taa ghafla alitokea karunguyeye amevalishwa nguo akiwa mkubwa kuliko umbo la kawaida. Baada ya mganga huyo kumuona alimshika na kumpasua, ndipo alipotoa fuvu hilo tumboni, sarafu za zamani na za sasa sh. 4,000 dawa ya kienyeji na ndege wawili wadogo walioruka kusikojulikana mara baada ya mnyama huyo kupasuliwa.
Kamanda Matei, alisema mganga ni mwenyeji wa Korogwe, Tanga na alihamia Arusha Desemba mwaka jana na kupanga katika nyumba ya Mzee Jeremiah Machupa akijishughulisha na biashara ya uganga wa kienyeji. Aliongeza kuwa hata hivyo alipopekua jalada lenye majina ya waganga na wataalamu wa tiba asilia waliosajiliwa kihalali lililoko ofisini kwake, hakuona jina la mganga huyo. Kamanda Matei, alisema hivi sasa polisi wanaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na madaktari ili kubaini kichwa hicho ni cha nani na aliuawa au kufa lini ili kupata taarifa sahihi.
Alisema Jeshi lake linamshikilia mganga huyo huku taratibu za upelelezi zikiendelea na kwamba uchunguzi ukikamilika mganga atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kukutwa na fuvu la kichwa cha mtu. Tukio hilo limevuta hisia za wakazi wengi wa jiji la Arusha na maeneo ya jirani jambo liliwafanya kuingiwa na hofu kubwa kufuatia matukio ya watu kuuawa na kunyofolewa viungo vyao ikiwemo mauaji ya maalbino kuongezeka mjini Arusha.
Tukio hili pia linaelekea kufanana na l;ile lilitokea hivi karibuni jijini Dar es Salaam, baada ya kijana Ramadhan Mussa (18) kukamatwa akiwa na kichwa cha mtoto Salome Yohana (3) akijaribu kuingia nacho katika hospitali ya Taifa Muhimbili. Kijana Ramadha na mama yake Hadija Seleman (38) juzi walisomewa mashitaka ya mauaji katika Mahakama ya Kisutu.
Baada ya kusomwa mashitaka hayo, upande wa mshitaka uliieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo unahitajika uchunguzi wa kina kutokana na mazingira yake. Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Mei 19 mwaka huu.Habari hii na Magesa Magesa

No comments: