Friday, May 15, 2009

y, May 15, 2009 |
Kesi ya Manji dhidi serikali kusikilizwa Julai.


Na Sadick Mtulya
GODWIN Muganyizi, wakili wa mkurugenzi wa kampuni ya Quality Group Ltd, jana alikwamisha usikilizwaji wa kesi dhidi ya Manji na serikali.
Kesi hiyo namba 265/2008 inayosikilizwa na Jaji Richard Mziray, ilifunguliwa na Manji Novemba 7, 2008 katika Mahakama Kuu
Kitengo cha Ardhi na kuanza kusikilizwa Februari 11, 2009.
Manji anaishtaki serikali akiidai fidia ya Dola 29, 694, 750 za Kimarekani baada ya kumzuia kuendeleza shughuli za ujenzi katika kiwanja namba 2199, kitalu namba 6 kilicho katika makutano ya Barabara ya Samora na Mkwepu. Kiwanja hicho aliuziwa na serikali.
Jana Muganyizi alifika mahakamani hapo, lakini akaieleza mahakama kuwa asingeweza kuendelea na kesi hiyo kwa kuwa amepata udhuru.
Katika maombi yake mfanyabiashara huyo anataka serikali imlipe fidia hiyo pamoja na riba ya asilimia 12, gharama zote za kesi hiyo, kulisafisha jina lake pamoja na gharama nyingine kadri mahakama itakavyoona zinafaa.
Mchanganuo wa fidia hiyo ni kuwa, Manji anataka alipwe dola 23, 694, 750 za Kimarekani kama hasara aliyoipata kutokana na hatua ya ujenzi aliyokuwa amefikia, na Dola 6,000,000 za Kimarekani kama fidia kutokana na kuchafuliwa jina lake, kampuni na biashara zake.
Agosti 26, 2006 serikali kupitia Wizara ya Utalii na Mali Asili ilimsimamisha Manji kuendelea na ujenzi katika kiwanja hicho kutokana na Sheria Namba 23(1) ya kutotaka kubadilisha mandhari ya maeneo ya kihistoria
Katika hati ya mashtaka, Wakili Muganyizi kwa niaba ya Manji, amemshitaki katibu mkuu wa Wizara ya Ardhi na Makazi pamoja na Mwanasheria Mkuu.
Hati hiyo inasema katibu mkuu huyo anashtakiwa kwa kuwa ndiye aliyetangaza zabuni ya kuuza kiwanja hicho ambacho alikinunua kwa fedha taslim Sh295 milioni.
Manji anadai kuwa alihalalishwa kumiliki kiwanja hicho na kupewa hati namba 186166/102 baada ya kushinda zabuni iliyotangazwa na serikali kupitia wizara hiyo.
Pia anadai Novemba 30, 2005, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lilimuidhinisha kama mmiliki halali wa jengo hilo ambalo kwa wakati huo lilikuwa likikaliwa na mpangaji aliyejulikana kwa jina la Shekigendo Simon.
Manji anadai kuwa Februari 14, 2006 Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilimtaka kuliendeleza jengo kwa kubadilisha aina ya jengo alilokuwa akitaka kulijenga la ghorofa 20 na kama asingefanya hivyo angetozwa faini ya kutoendeleza kiwanja na hiyo ilikuwa ni amri kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hati hiyo, inasema uamuzi wa Manji kudai fidia hiyo umetokana na serikali kutomjibu barua yake aliyowapelekea na kutotoa maelezo kwa wananchi kuhusu ukweli wa tatizo hilo. Kesi hiyo itasikilizwa tena Julai Mosi mwaka huu.
Habari Kwa Hisani: www.mwananchi.co.tz

No comments: