Wednesday, May 13, 2009

Mawazo Mazuri Ya Nyerere Yalinivuta Kusoma UDSM-Museveni.
Rais wa Uganda, YoweriMuseveni, amesema aliamua kuja kusoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kutokana na mawazo mazuri aliyokuwanayo hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema Mwalimu Nyerere alifanya mambo mengi ikiwemo kuendesha mapambano ya kuzikomboa nchi za Afrika.
Aliongeza kuwa wakati huo nchini mwake hapakuwa na watu wanaoona kama alivyokuwa anaona mambo mbalimbali Mwalimu Nyerere.
"Nchini mwangu kulikuwa na watu ambao hawakuwa na miwani machoni mwao hivyo walikuwa hawaoni," alisema.
Rais Museveni katika hotuba yake alitumia muda mwingi kuelezea athari za ukoloni katika nchi za Afrika na namna ya Waafrika wenyewe wanavyoweza kutumia raslimali zao kujiletea maendeleo.
Alisema nchi nyingi za Afrika zina rasmilimali nyingi ambazo zingetosha kusomesha wananchi wao, lakini tatizo bado wanakabiliwa na fikra za kutawaliwa na Wakoloni hali inayowafanya wasijiamini.
Alitoa mfano wa nchi ya Demokrasia ya Congo (DRC) ambayo alisema ina raslimali nyingi kuliko watu wake na kwamba nchi hiyo wananchi wake wangestahili kukaa bila kufanya kazi yoyote.
Hata hivyo, alisema pamoja na nchi hiyo kujaliwa mali nyingi, lakini bado masikini kuliko India ambayo ina watu wengi, lakini raslimali chache.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema uamuzi wa kugawa Chuo hicho ulifanywa na Baraza la Magavana la Chuo hicho katika mkutano wao uliofanyika mwaka jana.
Alisema Baraza la Chuo lilipitisha kuwa ifikapo Julai mwaka huu Chuo hicho kipya kiwe kimeanza kufanya kazi.
Alisema Mkuu wa chuo hicho kipya ameshateuliwa pamoja na wakurugenzi na kwamba mwezi ujao watakuwa wamemaliza uteuzi wa nafasi ya Naibu Mkuu wa Chuo.
Aliongeza kuwa Rais Museveni ni miongoni mwa wanafunzi wa mwanzo waliosoma chuoni hapo na kwamba mtu mwingine ambaye hivi sasa ni kiongozi wa nchi ni Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Habari Kwa Hisani: Nipashe

No comments: