Wednesday, May 13, 2009

Migodi 70 Ya Tanzanite Yasimama Kazi



Migodi zaidi ya 70 ya madini aina ya tanzanite iliyopo Mererani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, imesimama kufanya kazi kwa zaidi ya siku 30 baada ya transfoma ya umeme kulipuka.
Kutokana na hali hiyo, wamiliki wa migodi hiyo wamekuwa wakipata hasara ya mamilioni baada ya kusimama kwa shughuli za uzalishaji kwani kwa siku hutumia zaidi ya Sh 500,000 kutokana na kulisha wafanyakazi na gharama nyingine.
Akizungumza na gazeti hili katika eneo la tukio, mmiliki wa mgodi uliopo kitalu B, John Mkenga alisema transfoma hiyo imekuwa ikiharibika mara kwa mara, lakini hakuna jitihada zinazochukuliwa na uongozi wa Shirika la Umeme (Tanesco) juu ya hali hiyo ambayo inawaweka katika hali ngumu kwa sasa.
Alisema transfoma imekuwa ikifanyiwa ukarabati mara inapoharibika, lakini haichukui muda mrefu inaharibika tena na uongozi wa Tanesco Kanda ya Arusha unalifahamu hilo, lakini hakuna jitihada zinazofanyika juu ya hilo.
Alisema na kuishauri Tanesco kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wanaweka transfoma nyingine mpya ili kuondoa wingu la tuhuma kuwa shirika hilo linawahujumu wachimbaji wadogo kwa kushirikiana na wachimbaji wakubwa. “Hivi sasa hatufanyi kazi na tunalipa watu na kulisha watu bila kazi hiyo ni gharama kubwa hivyo tunaiomba Tanesco kuwa na huruma na wachimbaji wadogo kwa kuwawekea transfoma mpya yenye uwezo wa kuhimili mahitaji ya eneo hilo,” alisema Mkenga.
Mchimbaji mwingine, Julius Mollel aliilaumu Tanesco moja kwa moja kwa uzembe huo uliochukua zaidi ya siku 30 na kueleza kuwa viongozi wa shirika hilo wanapaswa kuwajibika juu ya hilo. Alisema transfoma imeharibika muda huo na Tanesco inalijua hilo, lakini hakuna jitihada za kushughulikia suala hilo na kuwaona wachimbaji wadogo kama raia wasiokuwa na maana kwao.
Mmoja wa wafanyakazi wa Tanesco aliyeomba kutotajwa jina lake kwa madai kuwa si msemaji wa shirika hilo, alikiri kuharibika mara kwa mara kwa transfoma hiyo na kueleza kuwa chombo hicho kimepelekwa tena kufanyiwa ukarabati katika kiwanda cha Tanalec kilichopo mjini Arusha.
Alisema transfoma hiyo ambayo imeshatengamaa, inashindwa kuchukuliwa kutokana na Tanesco kudaiwa mamilioni ya fedha na kiwanda hicho hatua inayokuwa ngumu zaidi. Juhudi za kumpata Kaimu Meneja wa Tanesco Kanda ya Mkoa wa Arusha na Manyara, Victor Massawe hazikuzaa matunda.
Habari Kwa Hisani Ya John Mhala, Mererani

No comments: