Friday, May 15, 2009

Nyumba zilizoharibika Mbagala sasa ni 7,000


Idadi ya nyumba zilizoharibiwa na milipuko ya mabomu katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Mbagala, jijini Dar es Salaam mwezi uliopita, imeongezeka kutoka nyumba 4,636 hadi nyumba 7,000.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, alisema idadi hiyo imebainishwa na wataalamu wanaofanya tathmini ya nyumba na mali katika eneo la Mbagala.
Alisema zoezi la tathmini linaendelea vizuri na kwamba amewaongezea wataalamu wanaofanya tathmini vifaa muhimu kama kompyuta ndogo ili kurahisisha kazi hiyo.
Hata hivyo, Lukuvi ameonya kuwa serikali haitawalipa wananchi ambao hawajapata madhara
yoyote kutokana na milipuko hiyo.
“Maana kuna watu wamekaa kule hawaendi kazini na hawajaharibikiwa hata na kikombe cha chai wanasubiri kufanyiwa tathmini…zoezi hili ni kwa ajili ya wananchi walioathirika tu,” alifafanua.
Alisema taarifa ya awali kuhusu nyumba zilizoathirika itatolewa mwishoni mwa wiki hii.
Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo, amewatahadharisha wananchi wa Mbagala na wakazi wa maeneo ya jirani na eneo ilipotokea milipuko hiyo kutogusa chuma chochote wasichokijua kwa kuwa vyuma vingine ni hatari.
Alisema eneo hilo bado lina vitu vingi vya hatari ambavyo vimesambaa na kwamba wananchi wanatakiwa kuwa makini.
“Kwa sasa hivi tunafanya usafi kuhakikisha takataka zote zinaondoka kwa sababu si salama, tumewaonya wananchi wasiguse kitu chochote wanachokitilia shaka ila watoe taarifa kwa wanajeshi walio katika eneo hilo,” alisema.
Kuhusu mlipuko wa juzi jioni katika eneo hilo, alisema wanajeshi walilipua bomu lililokuwa halijalipuka baada ya kulibaini.
Alisema wataendelea kuteketeza mabaki yote yatakayopatikana, lakini watakuwa wanatoa taarifa kwa wananchi wa karibu na kambi hiyo.
Katika hatua nyingine, ubalozi wa Marekani umetoa msaada wa fedha wa Sh. milioni 65 kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa milipuko hiyo. Kaimu balozi wa Marekani nchini, Larry Andre, alitangaza kutoa msaada huo jana na kuahidi kuendelea kuisaidia serikali kutokana na janga hilo.
  • Na Marekani yatoa msaada wa mil. 65/-

Habari Kwa Hisani: Na Restuta James

No comments: