Wednesday, May 13, 2009

Tuhuma Za Magufuli Zamng'oa Kamanda Wa Polisi Mwanga
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, John Magufuli



Na Daniel Mjema, Moshi
JESHI la Polisi limemuondoa mkuu wa polisi wa wilaya ya Mwanga (OCD), Evance Mwijage siku chache baada ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, John Magufuli kumweleza ofisa huyo mwandamizi kuwa anatuhumiwa kwa rushwa na wananchi.
Magufuli alimweleza waziwazi OCD huyo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika wiki iliyopita kuwa wananchi wanamtuhumu kwa kupokea rushwa kutoka kwa wavuvi haramu na habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa Kamanda Mwijage sasa hayupo tena Mwanga.
Kamanda wa polisi mkoa wa Kilimanjaro, Lucas Ng’hoboko alithibitisha kuondolewa kwa OCD huyo akisema hilo limefanyika ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotajwa dhidi yake kwa kuwa ni nzito.
Ng’hoboko alisema nafasi ya OCD huyo itachukuliwa na SP Ramadhan aliyekuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ingawa hakusema hatima ya polisi wa vyeo vya chini wa Mwanga ambao pia walilalamikiwa na wananchi.
Hivi karibuni katika mkutano wa hadhara, uliofanyika katika Kijiji cha Kagongo, Waziri
Magufuli alisema polisi wa Mwanga wanahusishwa sana na rushwa na kwamba ndio maana
hawakushirikishwa katika operesheni iliyoendeshwa katika bwawa hilo ya kupambana na wavuvi haramu.
Baada ya kutamka maneno hayo, Waziri Magufuli alimgeukia OCD Mwijage, aliyekuwa amekaa meza kuu na kumpasulia hadharani kuwa hata yeye wananchi wanamtuhumu na kwamba yeye (Magufuli) alipokea 'meseji' nyingi za simu zinazomtuhumu kamanda huyo wa polisi.
Waziri Magufuli alisema wananchi wamewataja waziwazi polisi wa Mwanga kuhusika na uchafu huo na aliahidi kwenda kuwashitaki kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema, kwamba wamekuwa kikwazo cha ulinzi shirikishi.
Kutokana na uzito wa tuhuma hizo, Jeshi la Polisi limeamua kumuondoa OCD Mwijega katika wilaya ya Mwanga na kumrudisha makao makuu ya mkoa wa Kilimanjaro ambako atapangiwa kazi nyingine.
Mbali na Waziri Magufuli, naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe alisema wavuvi haramu katika bwawa hilo wameunda umoja wao mithili ya vyama vya kuweka na kukopa, Saccos, ambacho alidai kinatumika kuwahonga polisi.
“Nilipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii nilileta boti la doria, lakini likalipuliwa
kwa baruti, kibaya zaidi hapa kuna umoja wa wavuvi haramu, wana Saccos, wanachanga pesa, wanakwenda Mwanga, wanawahonga polisi,” alisema.
Profesa Maghembe alisema polisi wa Mwanga wamekuwa wakipewa rushwa ya hadi
Sh400,000 kiasi kwamba makokoro yaliyokuwa yakikamatwa yalikuwa hayachomwi
moto na badala yake yanarudishwa kwa wavuvi haramu.
Kwa mujibu wa Profesa Maghembe, mtandao huo ndio uliolipua boti la serikali la doria na kwamba baada ya polisi kupewa hongo, wamekuwa wakifunga macho huku samaki wadogo wakisafirishwa mbele yao.
Tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Waziri Magufuli amekuwa akipambana na uvuvi haramu unaofanyika kwenye maziwa na bahari na hivi karibuni ushirikiano baina ya Tanzania na nchi nyingine zilizo pwani ya Bahari ya Hindi ulisaidia kukamata samaki zaidi ya tani 270 aina ya tuna kwenye pwani ya Tanzania.

No comments: