Friday, May 15, 2009

Simu Za Mkononi Kuanza Kubanwa Julai.

Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTs) katika Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dk. Zaipuna Yonah akizungumza wakati wa maadhisho ya siku ya Tekinolojia ya Habari na mawasiliano Duniani (TEKNOHAMA) jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma.


*********************
Kuanzia Julai mosi mwaka huu, watumiaji wote wa simu za mkononi nchini watatakiwa kusajili kadi na simu zao upya kwenye kampuni za huduma za simu ili ziweze kuchukua taarifa binafsi za wateja. Taarifa binafsi zitawezesha kampuni za simu na serikali kufahamu kila mtu anayemiliki kadi ya simu ili kudhibiti matumizi mabaya ya simu hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma, alisema jana Dar es Salaam kuwa uandikishaji wa kadi utafanyika kwa miezi sita na ifikapo Desemba mwaka huu, kadi ambazo zitakuwa hazijaandikishwa hazitafanya kazi. Profesa Nkoma ambaye alikuwa akizungumza katika semina ya wahariri wa vyombo vya habari kuhusu Wiki ya Mawasiliano na Habarijamii Duniani iliyoanza jana hadi Jumapili, alisema kuanzia muda huo, kadi za simu zitauzwa kwa utaratibu maalumu.
Alisema badala ya kadi kuuzwa kiholela mtaani, kampuni za simu zitalazimika kutafuta mawakala maalumu ambao watafahamika na watapewa namba za utambuzi kutoka TCRA ili waweze kufanya kazi kwa kufuata maelekezo ya mamlaka hiyo. Profesa Nkoma alisema baada ya kuandikishwa, wakala hao watapokea maombi mapya ya kadi za simu na kuchukua taarifa za wenye simu na kuzipeleka kwenye kampuni za simu.
Kampuni za simu nazo zitatoa huduma hiyo. Alisema taarifa zitakazohitajika ni zile ambazo zipo kwenye vitambulisho vya watumiaji simu na kama vitambulisho vitakuwa havina picha, mteja atalazimika kupeleka picha kwenye kampuni ya simu au wakala wake. “Baada ya miezi sita kupita, simu zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa hazitafanya kazi,” alisema na kuongeza kuwa kazi hiyo itafanywa kwa umakini baina ya mamlaka hiyo, serikali na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).
Alisema lengo ni kudhibiti matumizi mabaya ya simu ambapo watu wengine wamekuwa wakitumia simu hizo kufanya udanganyifu na uhalifu, lakini baada ya mpango huo kukamilika, watu hao watadhibitiwa. Profesa Nkoma alisema hata simu za mkononi zitatambulika, hivyo kama simu ikiibwa, mmiliki akitoa taarifa simu yake itafungwa hivyo mwizi hataitumia. Alisema TCRA ilianza kwa kuzuia matumizi ya namba binafsi Machi mosi mwaka huu na hatua hiyo ilisaidia kuzuia vitendo vingi visivyo vya kawaida katika jamii.
Tanzania ina jumla ya kadi za simu milioni 13. Kaulimbiu ya mwaka huu ni kumlinda mtoto dhidi ya athari za matumizi ya mtandao wa intaneti.
Habari Na Picha Kwa Hisani: Faraja Mgwabati/Salhim Shao.

No comments: