Wednesday, May 13, 2009

" Nawapa Siku 90 Kukamilisha Michango...." Pinda


NAWAPA SIKU 90 KUKAMILISHA MICHANGO YA MAJI - PINDA

*Asema wasipokamilisha, mradi uhamishiwe kijiji kingine



WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewapa miezi mitatu wakazi wa kijiji cha Kilyamatundu kata ya Kipeta wawe wamekamilisha kutoa michango kwa ajili ya mradi wa maji safi la sivyo utahamishiwa katika kijiji kingine.



Alitoa kauli hiyo jana mchana (Jumatatu, Mei 11, 2009) wakati akihutubia mkutano wa hadhara na kujibu maswali ya wakazi wa kata hiyo ambako alikuwa katika siku ya pili ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa.



Waziri Mkuu alishangazwa na ugumu wa wakazi hao kuchelewa kukamilisha michango wakati wana mifugo mingi na wamevuna mpunga kwa wingi, jambo ambalo alisema lingeweza kuwasaidia kumudu michango ya sh. 2,000 kila mwanakijiji.



“Serikali imetenga sh. milioni 150 kwa ajili ya mradi huu. Haiwezekani tangu mwaka 2004 muwe mmechangia sh. 500,000 tu… sisi kama Serikali tunaandaa mipango na tunataka umiliki wa wananchi katika miradi kama hii, ndiyo maana mnaombwa mchangie asilimia tano tu ya gharama zote ambayo ni sh. milioni 7.5/-,” alisema.



Alisema kuna vijiji zaidi ya 100 katika wilaya hiyo ambavyo vinahitaji kupatiwa miradi ya maji safi lakini ni vijiji 10 tu ambavyo viliteuliwa kupatiwa mradi huo. “Huu ni mwezi Mei, ifikapo Agosti 31, kama hawajakamilisha michango yao, Mkurugenzi warudishie michango yao, na upeleke huu mradi kwenye kijiji kingine,” alisema Waziri Mkuu.



Akijibu maswali ya wananchi, Waziri Mkuu aliwaagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Bw. Thobias Sijabaje na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Mussa Zungiza wafuatilie madai ya ujenzi hafifu wa shule ya sekondari ambayo wananchi walisema ujenzi wake umelipuliwa. “DC wenu ni mpya lakini itabidi aje na Mkurugenzi watafute ni kwa nini hadhi ya majengo hailingani na thamani halisi ya fedha,” alisema.



Akijibu maombi yao ya kupatiwa mradi wa umwagiliaji kwenye kutoka mto Momba unaomwaga maji yake katika ziwa Rukwa, Waziri Mkuu aliwaagiza viongozi wa halmashauri hiyo wafuatilie kama mradi huo upo na kama ulishafanyiwa upembuzi yakinifu kama wananchi hao wanavyodai.

Leo Waziri Mkuu anaanza ziara ya siku mbili katika jimbo lake la Mpanda Mashariki kwa kutembelea kata za Muze na Mamba ambako atafanya mikutano ya hadhara na kukabidhi kasiki ya kutunzia fedha kwa SACCOS ya Muze.



IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMANNE, MEI 12, 2009.

No comments: