kubenea wa gazeti la mwanahalisi matatani
JK akimfariji mhariri wa gazeti la mwanahalisi, saeed kubenea, baada ya kujeruhiwa kwa kumwagiwa tindi kali mwaka jana
MAHAKAMA Kuu imewaamuru Mhariri, msambazaji, mchapishaji wa gazeti la Mwanahalisi kumlipa Sh Bilioni tatu Mfanyabiashara Rostam Aziz kwa tuhuma za kuchapisha habari ya kumkashfu kwa kumhusisha kushiriki kwenye tuhuma za kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond.
Uamuzi huo ulitolewa April 30, Mwaka huu na Jaji wa mahakama hiyo Robert Makaramba, baada ya walalamikiwa kushindwa kutoa utetezi dhidi ya kesi iliyofunguliwa na Rostam ambaye pia ni Mbunge wa Igunga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika kesi hiyo, Rostam alilifungulia kesi Gazeti hilo la Mwanahalisi baada ya kuchapisha taarifa ya kumkashifu wakili wa Rostam.
Katika uamuzi wake Jaji Makaramba alisema kuwa baada ya Rostamu kufungua kesi hiyo Aprili 22, Mwaka jana, walalamikiwa walishindwa kuwasilisha utetezi wao ndani ya siku 21 kwa mujibu wa sheria kitendo kilichomfanya wakili Kennedy Fungamtama anayemtetea Rostam kuiomba mahakama hiyo kutumia vifungu vilivyoko chini ya sheria ya mwenendo wa makosa ya madai kutoa hukumu dhidi ya walalamikiwa, ombi ambalo lilikubaliwa na jaji huyo.
Mbali na kulitaka gazeti hilo kulipa fedha hizo, Mahakama hiyo pia imeliamuru gazeti hilo kukanusha tuhuma hizo na kuomba radhi katika ukurasa wa mbele wa gazeti hilo haraka iwezekanavyo.
Pia mahakama imeitaka gazeti hilo pamoja na mawakala wake kutokana na kulipa kiasi hicho cha fedha kwa kumkashifu mlalamikaji, pia linatakiwa lilipe asilimia 12 ya kiasi hicho kama gharama za kesi.
Naye wakili Kennedy Fungamtama, ambaye anamtetea Rostam amelipa gazeti hilo siku 14 za kutimiza amri hizo za mahakama la sivyo watachukua hatua kwa lengo la kumlinda mteja wake.
Hata hivyo Wakili Gabriel Mnyele ambaye analiwakilisha gazeti hilo katika shauri hilo, alisema hakubaliani na uamuzi huo wa Mahakama Kuu, hivyo upande wa walalamikiwa utakata rufaa.
Katika kesi hiyo Rostam alilalamika kuwa habari hiyo ilimhusisha yeye na vitendo vya rushwa, mtu asiye mwaminifu kutokana na kuhusishwa na habari hiyo kuwa alihusika kwenye mpango wa kufanya ushawishi dhidi ya kampuni hiyo.
Katika kesi yake alisema pamoja na kutokuwa ushahidi wa yeye kuhusika kwa namna yeyote ile na madai yaliyokuwemo kwenye habari hiyo lakini gazeti hilo liliendelea kuchapisha habari nyingine kwenye toleo namba 085 la Februari 20 hadi 26 mwaka jana likimhusisha mlalamikaji na kampuni hiyo ya Richmond.
Katika kesi hiyo Rostam alisema gazeti hilo lilichapisha tena habari yenye kichwa cha habari kuwa ‘Kikwete amtosha Lowassa’ ambako alitajwa mlalamikaji na biashara zake kuwa alihusika alivyoshiriki kwenye suala la Richmond.
Alisema kwa habari hiyo yeye kama mbunge na mfanyabiashara aliathirika kwa kiasi kikubwa kwani utu wake umedharirishwa mbele ya jamii na imesababisha aonekane mtu asiye mwadilifu na anayekabiliwa na kashfa kadhaa.
Rostam alidai kuwa, kutokana na tuhuma hizo za uongo zimemdharirisha hasa likizingatiwa kuwa kabla ya tuhuma hizo alikuwa ni mtu aliyeheshimika kama raia mwema, mfanyabiashara na mwanasiasa.
No comments:
Post a Comment