polisi wetu watunukiwa nishani Darfur kwa utumishi uliotukuka
ya pamoja na Hassan Gibril kulia mkuu wa vikosi vya usalama vya umoja wa mataifa.
Picha na habari na Mohammed Ramah Mhina,
wa Jeshi la Polisi akiwa DARFUR SUDAN,
Umoja wa Mataifa Sehemu ya Afrika unaosimamia masuala ya Usalama eneo la Darfur nchini Sudan, UNAMID, umewatunukia Askari Polisi wa Tanzania Nishani za Ulinzi wa Amani kutokana na Utii na Uaminifu wao katika masuala ya kiusalama.
Akiwavisha nishani hizo, Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jenerali Henry Anyidoho, aliwapongeza Askari wa Tanzania kwa nidhamu na uwajibikaji wao wa kiwango cha juu na mfano wa kuigwa na Polisi wa Mataifa mengine duniani.
Jenerali Anyidoho ambaye pia aliambatana na Mkuu wa Utawala wa UNAMID Bw. Wolfgang Weiszsgger, alisema kuwa nidhamu na uwaminifu unaonyeshwa na Askari Polisi wa Tanzania ni kielelezo cha matunda mema yaliyoachwa Mwanzilishi wa Taifa hilo Hayati Mwl Julias Nyerere ambaye ametunukiwa jina la Baba wa Taifa.
Huku akishangiliwa kwa vifijo na nderemo wakati wote wa hotuba yake, Jenerali Anyidoho aliwataka askari hao kuzivaa nishani hizo wakati wote huku wakiwa vifua mbele kwani mchango wao kwa Umoja wa Mataifa ni mkubwa na muhimu na wenye kuleta nuru ya matumaini katika Darfur.
Jenerali Anyidoho amesema anajisikia faraja na furaha isiyo kifani kuwa yupo katikati ya “Watoto wa Nyerere” aliye Tochi na Mwanga wa amani kwa waliokata tamaa Barani Afrika.
Ameishukuru sana Tanzania kwa kuwajali wenye shida kama Wananchi wa eneo la Darfur nchini Sudan na umuhimu wa kutuma askari wake kwenda kulinda amani katika mazingira magumu.
Awali, akimkaribisha Jenerali Anyidoho, Kamanda wa Polisi wa Tanzania katika Darfur Mrakibu Msaidizi (ASP) Jemes Kasusura, alisema kuwa pamoja na hali ngumu ya kiuchumi na uchache wa askari nchini Tanzania, lakini askari wake wamekuwa wakishiriki katika misheni mbalimbali za kulinda amani katika nchi zenye migogoro ndani na nje ya Bara la Afrika.
Kasusura amezitaja baadhi ya nchi ambazo Askari wa Tanzania wameshashiriki kulinda amani kuwa ni Kosovo, Sierra Leone, Angola, Msumbiji na nchi nyingine nyingi ambapo baadhi ya nchi hizo hivi sasa zina amani.
Amesema tangu enzi za Mwl Nyerere, Watanzania wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa baadhi ya nchi zilizokuwa zikitawaliwa zinapata uhuru na kuwawezesha kuwa na utawala wa kidemokrasia.
Wengine waliovishwa nishani kama hizo ni Askari Polisi kutoka nchini Burundi ambao pia ni sehemu ya askari wa kulinda amani kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
No comments:
Post a Comment