Friday, March 19, 2010

MABANGO YA KANISA LA KAKOBE YAONDOLEWA
Sasa hivi katika pita yangu mitaa ya Mlimani city huku Mwenge nimekuta mafundi wa TANESCO na kampuni moja toka JAPAN wanayaondoa mabango ya kanisa la FULL GOSPEL FELLOW SHIP ambalo linaongozwa na Mchungaji Zacharia Kakobe chini ya ulinzi mkali wa polisi bila shaka kuruhusu kupitishwa kwa waya za umeme.

Juu na chini ni mabango ya kanisa la Kakobe yakiondolewa kwa winchi
-------------------------
HABARI KAMILI
Hatua hii inakuja baada ya serikali kuliruhusu Shirika la Umeme (Tanesco) kuendelea na mradi wa kupitisha nyaya za umeme wa msongo wa 132KV juu ya eneo hilo, baada ya ya waumini kulinda majengo ya Kanisa hilo la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) kwa takribani miezi mitatu

Waumini hao walikuwa wakikesha usiku na mchana kwa lengo la kuzuia wafanyakazi wa Tanesco kupitisha nyaya hizo juu ya kiwanja cha kanisa hilo lililo jirani na eneo la Mwenge wilayani Kinondoni baada ya mkuu wa FGBF, Askofu Zacharia Kakobe kupinga mradi huo na kutangaza eneo hilo kuwa la hatari kwa wafanyakazi wa shirika hilo la ugavi wa umeme.

Askofu Kakobe anadai kuwa mradi huo wa thamani ya Sh34 bilioni kutoka serikali ya Japan haufai kupitishwa juu ya eneo la kanisa hilo kwa kuwa ni hatari kwa afya za waumini wake na unaweza kuharibu mawasiliano ya ndani wakati wa ibada, ambazo alisema hurekodiwa wakati zikiendelea na pia kudai kuwa utavuruga mawimbi ya televisheni kwa kuwa kanisa hilo lina mpango wa kujenga studio ya runinga.

Askofu huyo alidai mradi huo ulipingwa na wakazi wa maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ndio maana ukakwepeshwa hivyo anataka Tanesco pia ikwepeshe nyaya zinazotakiwa kupita juu ya kanisa lake lililo kando ya Barabara ya Sam Nujoma.

Lakini Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja jana alisema kuwa serikali imejiridhisha kuwa mradi huo hautakuwa na athari za kimazingira na afya ya binadamu na hivyo kutupilia mbali ombi la Askofu Kakobe la kutaka nyaya hizo zipitishwe katikati ya Barabara ya Sam Nujoma.

Ngeleja, ambaye wizara yake ilifanya vikao kadhaa na uongozi wa FGBF, alisema eneo la katikati ya barabara hiyo haliwezi kutumika kwa ajili ya nyaya hizo kwa kuwa tayari lina nguzo za taa za barabarani na kuongeza kuwa eneo hilo la kati linakusudiwa kutumika kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kwa kasi.

By Mdau,Kashaga Boniphace


No comments: