Tuesday, August 26, 2008

`Canavaro` afiwa na mkewe



Mlinzi mahiri wa timu ya taifa, Taifa Stars ambaye pia ni mlinzi wa kutegemewa wa Yanga, Nadir Haroub `Canavaro`, amepata pigo baada ya mkewe Penina Mzunya aliyekuwa mjamzito kufariki dunia juzi wakati alipokuwa katika harakati za kujifungua katika Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini, Dar es Salaam jana na kudhibitishwa na mchezaji huyo zimeeleza kuwa mke huyo wa Canavaro alifariki Dunia alipokuwa akipewa msaada na madaktari katika kuyaokoa maisha yake kufuatia mtoto aliyekuwa tumboni kufariki kabla ya kuzaliwa.

Madaktari wakiwa katika harakati hizo za kumsaidia Penina ghafla hali ilibadilika, ambapo mke wa mchezaji huyo alipoteza maisha akiwa hospitalini hapo.

Imeelezwa kuwa Canavaro alipatiwa taarifa za msimba huo wa mkewe muda mfupi mara baada ya mchezo wa timu yake dhidi ya Prisons kumalizika, ambapo walishinda 4-0.

Akizungumza na Nipashe jana, Canavaro alisema kuwa ameumia sana kwa kumpoteza mke na mtoto, ambapo anaamini maumivu hayo hayatatoweka kwa muda mfupi.

``Ni kweli nimempoteza mke na mtoto wangu, nimeumia sana kwa tukio hili lakini naamini yote ni mipango ya mungu,`` alisema mchezaji huyo.

Shughuli za mazishi zinaendelea nyumbani kwa mke wa mchezaji huyo Sinza Legho, ambapo kuna uwezekano akasafirishwa kwenda jijini Arusha kwa maziko.

No comments: