Wednesday, August 20, 2008

Acheni kupiga Domo-Mkapa


Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu,Benjamin Mkapa,amewataka Watanzania kuacha kupiga domo badala yake watafute vipaji ili kulinda umoja na amani nchini.Amesema hayo jumapili wakati akizungumza kwenye sherehe ya Jubilei ya miaka 100 ya Ukristo Jimbo Katoliki la Singida zilizofanyika katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu.
Alisema pamoja na amani na utulivu uliopo hapa nchini,lakini bado kuna watu ambao wanatafuta mambo mabaya kwa lengo la kuwagawa Watanzania.Alisema Watanzania wana imani,dini na makabila mbalimbali,lakini ni vyema kila mtu akatumia kitu hicho kuwa pamoja na kudumisha amani na utulivu.Alikemea tabia ya baadhi ya watu kuwa na utamaduni wa kushabikia maneno ya vijiweni badala yake akawataka kuonyesha upendo na staha ili kuleta umoja miongoni mwa Watanzania.
Awali Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam,Polcarp Kardinali Pengo aliwataka Watanzania kupeleka ujumbe wa amani kwa wanaotumia silaha kwa lengo la kuvuruga amani. Alisisitiza kuwa kazi hiyo itaendelea mpaka mwisho wa dahari na kwamba miaka 100 ya Jimbo la Singida ni mwanzo wa kazi iliyopo mbele ya Kanisa la Singida na Kanisa la Ulimwengu mzima.Habari hii na Hudson Kazonta,Singida

No comments: