Tuesday, August 26, 2008

Serikali haijutii kukosa medali


By Beatrice Bandawe, Dodoma

Serikali imeibuka na kuitetea timu ya Tanzania iliyotoka mikono mitupu katika Michezo ya 29 ya Olimpiki iliyomalizika juzi jijini Beijing, China.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohammed Seif Khatib, alisema hayo, wakati akijibu swali bungeni kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika.

Khatibu, alikuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Bi. Nuru Awadhi Bafadhili, alihoji serikali inasemaje kuhusu aibu iliyopata Tanzania kutokana na kukosa medali katika michezo ya Olimpiki.

Alisema si aibu kutoka bila medali bali cha msingi ni Watanzania wenyewe kuijiimarisha ili waweze kushinda katika michezo inayokuja.

Katika michezo hiyo iliyomalizika, Tanzania ilipeleka timu za riadha na kuogelea, ambazo zote zilitoka mikono mitupu.

Katika swali jingine, Mbunge wa Mtera (CCM), John Malecela, alihoji serikali kwa nini isijenge Chuo cha Michezo kutokana na nchi nyingi zilizofanikiwa katika michezo serikali kuwajibika katika ujenzi badala ya kuwaachia watu binafsi.

Akijibu swali hilo, Khatibu, alisema serikali kwa kuthamini mchango wa michezo, imeshajenga chuo cha michezo cha Malya, jijini Mwanza.

Malecela aliuliza swali la nyongeza kutokana na swali lingine la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa, aliyehoji serikali ina mikakati gani maalumu ya kuwaandaa wanamichezo wake kushiriki katika michezo ya Olympic ili kuepuka aibu inayopata sasa.

Khatibu, alisema serikali inatambua umuhimu wa kuandaa wanamichezo wake na kuongeza kuwa hata Rais Jakaya Kikwete, wakati akilihutubia Bunge, wiki iliyopita, aliahidi kutafuta kocha wa riadha.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Bi. Mkiwa Kimwanga, alihoji kuwa kutokana na kuanzishwa kwa vituo mbalimbali binafsi vya kukuza na kuendeleza michezo, serikali inachukua hatua gani za ziada kuvisaidia vituo hivyo katika kutunza na kutimiza malengo hayo.

Akijibu Waziri Khatibu, alisema serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa ili kuvisaidia vituo hivyo katika kutunza na kutimiza malengo yake.

Aidha, katika nyakati tofauti imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za ziada kusaidia maendeleo ya michezo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri kwa Baraza la Michezo la taifa, BMT.

No comments: