libeneke la ze comedy na EATV aluta kontinyua
Waambiwa wasubiri kesi ya msingi
MAHAKAMA Kuu, Kitengo cha Biashara, imetupilia mbali maombi ya kikundi cha wachekeshaji maarufu kama Ze Comedy ya kutaka the East African Television (EATV) na walalamikiwa wengine wazuiliwe kuwabughudhi kwenye maonyesho yao kwa kutumia jina la Ze-Comedy.
Akisoma uamuzi katika mahakama hiyo leo , Jaji Mfawidhi Katharine Orio alisema kuwa baada ya kuangalia nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa hakuona miongoni mwa pande zote mbili mwenye haki ya kumiliki jina la Ze Comedy.
“Mahakama imetazama nyaraka zilizopo na imeona kwanza, hakuna mtu yoyote anayelimiliki jina la Ze Comedy linalogombewa kati ya waombaji (Ze Comedy) na mlalamikiwa wa kwanza (EATV) haki ya kulitumia jina hilo,” alisema Urio.
Jaji Orio alisema kuwa nyaraka zilizopo zinaonyesha kuwa EATV walishawasilisha maombi ya kuruhusiwa kutumia jina hilo, ambapo ofisi ya msajili haijatoa maamuzi juu ya maombi hayo.
Kwa upande mwingine, waombaji nao walipewa kibali cha kutumia jina hilo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai 1, mwaka jana hadi Juni 31, mwaka huu.
“Kibali hicho kimeshakwisha na hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa kuna maombi ya wao kuendelea kutumia jina hilo. Kama kuna maombi ya aina hiyo, basi mahakama haina taarifa,” alisema Orio.
Aidha Jaji alisema pia kuwa kinachoombwa kwenye kesi ya msingi vinafanana na maombi ya muda yaliyowasilishwa ambayo yanahitajika kutolewa uamuzi hivi sasa.
Alisema kuwa kuruhusu maombi ya waombaji yaliyopo ni sawa na kuamua kesi ya msingi iliyopo bila kupata ushahidi kutoka pande zote mbili, ambayo kisheria haikubaliki.
Alisema kutokana na kesi za namna hiyo kutokuwa nyingi hapa nchini mahakama imeona si wakati muafaka wa kutoa zuio kwa sasa na akaelekeza kesi ya msingi isikilizwe haraka ili mwenye haki aweze kupatikana.
“Mahakama imeona mpaka ilipofikia hakuna mtu yoyote mdai na mdaiwa atakayewajibika kulipa gharama zozote za kesi zilizojitokeza mpaka kesi ya msingi itakapotolewa hukumu, ” alisema Urio.
Baada ya kutoa uamuzi huo, jaji aliwaamuru mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja zao mahakamani hapo juu ya pingamizi zilizowasilishwa na walalamikiwa wakitaka kesi ya msingi itupiliwe mbali.
Aliwaamuru walalamikiwa kuwasilisha hoja zao tarehe 2, mwezi Ujao, ambapo walalamikaji watatakiwa kuwasilisha majibu yao tarehe 18, mwezi Septemba.
Jaji amesema atatoa uamuzi Octoba 21 juu ya pingamizi hizo.
Wasanii hao walikuwepo kusikiliza kesi yao ni Lucas Muhuvile ‘Joti’ Sekioni David ‘Seki’, Mujuni Sylivery ‘Mpoki’ , Isaya Mwakilasa ‘Wakuvanga’ Alex Chalamila ‘Mc Regan’ na Joseph Shamba ‘Vengu’Kundi hilo lilikuwa likifanya maigizo katika Kituo cha EATV, lakini baada ya kumaliza mkataba wake, limeingia katika matatizo baada ya kituo hicho kudai kuwa wao ndiyo wenye hakimiliki ya Ze Comedy.
Kundi hilo ambalo karibuni lilitangaza kudhaminiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia channel ya TBC1, lilifungua kesi katika mahakama kuu ya kitengo cha biashara, ikiishitaki EATV, ikidai Sh milioni 200 na kituo hicho kiwaache huru.
No comments:
Post a Comment