Wednesday, November 26, 2008

Orodha ya mawaziri waliowahi kushitakiwa...


2008-11-26 10:21:43
Na Muhibu Said

Jana historia ya mawaziri waliowahi kuitumikia serikali tangu uhuru iliiingia hatua mpya baada ya mawaziri wawili waandamizi wa serikali ya Awamu ya Tatu, Basil Mramba na Daniel Yona kushitakiwa mahakamani kwa makosa ya jinai na kufanya walikwisha kupanda kizimbani kwa makosa hayo kufikia sita.

Mawaziri hao, baadhi walikamatwa na kufikishwa mahakamani wakiwa madarakani na wengine walichukuliwa hatua hizo wakiwa nje ya madaraka.

Wa kwanza kukamatwa na kufikishwa mahakamani, ni aliyekuwa Waziri wa Sheria katika serikali ya Awamu ya Kwanza iliyokuwa chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, marehemu Abdallah Fundikira.

Fundikira alifikishwa mahakamani baada ya kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya rushwa na alichukuliwa hatua hiyo wakati huo akiwa madarakani katika miaka ya 1960, miaka michache tangu Tanganyika ipate uhuru. Hata hivyo, alishinda kesi.

Mwingine ni Venance Ngulla, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya awamu ya pili katika miaka ya 1990.

Ngulla alikamatwa na kufikishwa mahakamani katika miaka ya 1990, baada ya kutuhumiwa kumiliki gari katika njia zinazotatanisha. Hata hivyo, naye alishinda kesi.

Mwingine, ni aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Nalaila Kiula, katika serikali ya awamu ya pili, iliyokuwa chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi katika miaka ya 1990.

Kiula alikamatwa na kufikishwa mahakamani wakati wa utawala wa serikali ya Awamu ya Tatu uliokuwa chini ya uongozi wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kwa tuhuma za rushwa. Hata hivyo, naye pia alishinda kesi.

Katika miaka ya katikati ya 90, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya pili, Augustine Mrema naye alikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuwatuhumu hadharani baadhi ya viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali kwamba, wamepokea rushwa yenye thamani ya Sh. milioni 900. Hata hivyo, naye alishinda kesi.

  • SOURCE: Nipashe

No comments: