mdau willy edward amuomboleza nyaulawa
Mdau Willy Edward (hoto) akipokea cheti cha kuhitimu mafunzo na Mh. Richard Nyaulawa mwaka 1996. kati ni Mhariri mkuu wa majira, Sammy Makilla.
Kifo cha Nyaulawa kimenigusa, alikuwa mtu 'simpo' ALIZOEA kuitwa Nyaulawa, hususan wafanyakazi wa kampuni ya Business Times Limited (BTL) niliyowahi kuitumikia nikiwa mwandishi wa habari.
Ingawa kila nafsi itaonja mauti, lakini hakika kifo hakina huruma, kimetunyang'anya Richard Said Nyaulawa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa BTL (ambaye pia alikuwa mmiliki) na Mbunge wa Mbeya Vijijini.
Nyaulawa aliyefariki dunia alfajiri ya saa 9, Novemba 9, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 59, alikuwa kiongozi mwadilifu aliyechapa kazi kwa ufanisi mkubwa na hakuwa mpenda makuu.
Katika makala ya buriani ya gazeti la Uhuru toleo la leo Novemva 12, 2008, mwandishi Jacqueline Liana ambaye ni Naibu Mhariri Mtendaji wa Uhuru Publications Ltd (niliwahi kufanya naye kazi gazeti la Majira) amenikumbusha (mimi Willy Edward) matukio mengi kuhusu Nyaulawa.
Amenikumbusha kwamba wakati mmoja nikiwa kazini usiku nikisanifu kurasa za gazeti, Nyaulawa alinipigia simu katika chumba cha habari na kujitambulisha, hakika nilidhani ni mwandishi mwenzangu ananitania, niligoma kuzungumza naye nikimwambia: "Mimi ni mtu mdogo sana, Nyaulawa hawezi kunipigia simu, kwanza nakata unazidi kunichelewesha."
Nyaulawa alinisisitizia kwamba ni yeye ndiye alikuwa akipiga simu kuuliza kwanini gazeti lilikuwa halijafika kiwandani wakati huo kuchapishwa? Nilishikilia msimamo wangu kwamba Nyaulawa hawezi kunipigia simu.
(Wakati huo Mhariri Mkuu Majira alikuwa ni Mobhare Matinyi ambaye sasa anaishi Marekani). Punde si punde Nyaulawa aliendesha gari lake na kufika chumba cha habari nilikokuwa, baada ya kumuona sikuwa na ujanja zaidi ya kuamini alichokuwa akikisema kwenye simu, nikampa heshima yake aliyostahili na sote tukabaki tukicheka.
Hiyo inadhihirisha jinsi gani Nyaulawa alivyokuwa 'simpo' na asiyependa makuu, lakini alikuwa kiongozi makini.
Nyaulawa alianza kunifahamu zaidi kwa karibu mwaka 1996 wakati akinikabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya uandishi wa habari yaliyoandaliwa na Business Care Services (BCS), na nakumbuka mwaka huo ndio nilipewa zawadi ya mfanyakazi bora wa mwaka (wakati huo nikiandikia zaidi magazeti ya Dar Leo na Spoti Starehe) kabla ya kuhamishiwa rasmi Majira.
Vyumba vya habari vya magazeti ya BTL wakati huo vilisheheni waandishi mahiri wakiwamo aliyekuwa Mhariri Mtendaji, Sammy Makilla, Theophil Makunga, Joseph Kulangwa (sasa Mhariri Mkuu Majira), Faustine Rwambali, Jacqueline Liana, Masoud Sanani, Mobhare Matinyi, Irene Bwire (sasa mwandishi wa Waziri Mkuu), Juma Pinto (yupo Uingereza), Jesse Kwayu, Danny Mwakiteleko, Rachel Lugoe, Sopa Castico, Fatma Mwassa (msaidizi wa Mama Kikwete), Nyaronyo Kicheere, Ponsian Rwechungura, Lilian Kalaghe, Jabir Idrissa, Boniface Wambura, Samson Mbega, marehemu Nicky Maira, marehemu Conrad Danstan (kiona mbali) na wengine wengi.
Hakika marehemu Nyaulawa alikuwa mtu mtaratibu, lakini makini na muungwana na alikuwa kipenzi cha wengi.
Kwa heri Richard Nyaulawa!
Willy Edward
Senior PR Executive (Zain)
ZK Advertising.
No comments:
Post a Comment