Sunday, August 24, 2008

Mbowe aalikwa kwa
Obama ...

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA),Freeman Mbowe(Pichani),amealikwa kuhudhuria mkutano mkuu wa Chama cha Democratic,ambao utampitisha rasmi mgombea urais wa chama hicho,Seneta Barack Obama.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na CHADEMA jana na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Mahusiano ya Kimataifa wa chama hicho,John Mnyika, ilieleza kuwa akiwa nchini Marekani,Mbowe atahudhuria mkutano huo unaofanyika katika Jiji la Denver, Colorado,ambao utamuidhinisha Obama, ikiwa ni pamoja na kutangaza jina la mtu atakayekuwa mgombea mwenza wake.

“CHADEMA inapenda kuutaarifu umma wa Watanzania kwamba Mwenyekiti wetu ameondoka kwa ziara ya siku nne kwenda nchini Marekani,kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Chama cha Democratic, ambao utamwidhinisha kuwa mgombea urais wake,Barack Obama,pamoja na mgombea mwenza,”ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ya Mnyika imesema kwamba,Mbowe amealikwa kuhudhuria mkutano huo muhimu na taasisi ya National Democratic Institute(NDI),yenye dhamana ya kuandaa mkutano huo.
Miongoni mwa viongozi mashuhuri wa Kiafrika walioalikwa katika mkutano huo ni Waziri Mkuu wa Kenya,Raila Odinga,ambaye naye kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Kenya, amekubali mwaliko huo.

Akiwa huko,Mbowe atapata fursa ya kuhudhuria jukwaa la kimataifa la viongozi(Leadership Forum),ambalo huwakutanisha viongozi waandamizi mbalimbali duniani.
“Katika jukwaa hilo,kunakuwa na watu kama mabalozi, wanaharakati na wanasiasa waandamizi kutoka takriban mataifa 100 duniani,”iliongeza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza baada ya ziara hiyo ambayo itakamilika Agosti 28 mwaka huu,Mbowe atarejea nchini,na baada ya kurudi atazungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali ya mwelekeo wa taifa na chama chake.Habari na Kulwa Karedia


No comments: