Thursday, June 5, 2008

ONYO KUHUSU BAADHI YA BENDI KUWAONYESHA WANENGUAJI NUSU UCHI KATIKA MAJUKWAA YA MUZIKI..

Hivi karibuni Baraza la sanaa la Taifa limeshtushwa na kasi ya mmomonyoko wa maadili ya watanzania kwa baadhi ya bendi za muziki wa dansi nchini kutumia majukwaa ya dansi kwa makusudui kudhalilisha wanenguaji wa kike,kudhalilisha watazamaji na kuwaharibu watoto wadogo kwa baadhi ya wanenguaji wakiwa na vichupi na wanengfuaji kuonekana kuwa nusu utupu.


Baadhi ya wamiliki wa bendi wameiga tabia ya baadhi ya wanamuziki wa nchi jirani kwa kuonyesha wanenguaji nusu utupu.Tabia hiyo imechukuliwa kama biashara katika kumbi za maonyesho ya muziki na mbaya zaidi ni kwamba biashara hiyo haiishii hapo bali imewafikia watoto wadogo kwa kuona dhambi hiyo kupitia vyombo vya habar.


Hayo tumethibitisha katika ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na watendaji wa Baraza kati ya tarehe 24/5/2008 hadi tarehe 1/6/2008.BASATA linachukua fursa hii kuwaaasa wamiliki wa bendi zenye tabia hiyo kuacha mara moja na ikithibitika kuendelea kuvunja agizo hili,bendi hizo zitachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kuzifungia kufanya maonyesho au kuzifutia usajili.


Aidha tunawaomba wamiliki wa vyombo vya habari kuacha kuwaunga mkono wadhalilishaji hawa kwa kutoonyesha au kuchapisha picha za wanenguaji waliovaa vichupi ili kulinda maadili yetu ya kutoharibu kizazi chetu ambacho hivi sasa kinaharibiwa kwa kuonyesha watoto mambo ambayo hawastahili kuyaona katika umri walio nao.


Ni nafasi hii pia tunawaomba wanenguaji wakike kuacha kutumika kama chombo katika biashara za watu kwa kudhalilishwa utu wa mwanamke.Aidha BASATA linawaomba wanaharakati wa haki za binadamu,wanaharakati wa masuala ya wanawakae kutokaa kimya katika suala hili,kwani maadili ya watanzania yanapobomolewa umma wa watanzania ndio unaoteketea.


Pia wadau wa muziki tunawaomba zikatae bendi zinazoonyesha vichupi na wasiositiri mwili wa mwanamke hadi watakapobadili tabia hizo,tukiweka tafakari kuwa,watazamaji wangejisikiaje kama binti zao na dada zao wangecheza na vichupi mbele yao.


Tunaamini kuwa biashara ya muziki itafana kwa kuwa ubora wa muziki wenyewe unaoambatana na uzingatiaji wa maadili (mila desturi)na kamwe vichupi havitaupamba muziki mbovu kuwa muziki bora.
Imetolewa na
D.Lauwo
KAIMU KATIBU MTENDAJI
BASATA
2 JUNI,2008

No comments: