Monday, June 30, 2008

Asilimia Kubwa ya Majengo Bongo
Hatari Tupu

ZAIDI ya maghorofa 100 jijini Dar es Salaam yamebainika kuwa yalijengwa kinyume cha taratibu za ujenzi,Bunge limeelezwa,ripoti iliyoundwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa imesema.

Maghorofa hayo ni kati ya maghorofa 505 ambayo yalikaguliwa ambapo 147 yalikutwa hayana nyaraka za ujenzi.Lowassa aliunda tume baada ya jengo la Hoteli ya Chang’ombe Village Inn, Keko,Dar es Salaam kuanguka mwaka 2006 na kuua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa. Ilidaiwa kwamba ulikuwapo ukiukwaji katika ujenzi wake.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliliambia Bunge wakatyi akifunga hotuba yake ya bajeti kuwa tume hiyo ya Lowassa, ilibaini katika ukaguzi huo,kuwa maghorofa 81 yalikutwa yamekiuka masharti ya ujenzi huku maghorofa mengine 22 wenyewe hawakupatikana na yalikuwa yamejengwa bila kuzingatia sheria za ujenzi.Panda alisema maghorofa mengi yanayojengwa Dar es Salaam yanajengwa holela bila kufuata taratibu za ujenzi,hivyo kuyafanya kuwa hatari kwa maisha ya binadamu.

Alisema kama hatua za haraka hazitachukuliwa na serikali,kuna hatari ya watu wengi kupoteza maisha kwenye maghorofa hayo ambayo yanachipuka kama uyoga katikati ya Dar es Salaam, likiwamo eneo la Kariakoo.Alisema tukio la kuporomoka kwa ghorofa kulikotokea wiki iliyopita Kisutu, Dar es Salaam, ni uzembe wa baadhi ya watendaji wakiwamo wahandisi wa manispaa husika.Alisema kutokana na taarifa hiyo ya tume,serikali inaandaa utaratibu mzuri wa utekelezaji wake kuhakikisha maghorofa yanayojengwa yanakuwa bora na yanayofuata taratibu zote za ujenzi.
Habari hii imeandaliwa na
Msimbe Lukwangule

No comments: