Harare Miaka 21
Iliyopita..!
Jana yaweza kabisa kuwa ni mwanzo wa mwisho wa Mugabe. Jana Wazimbabwe wanafanyishiwa 'uchaguzi wa kitapeli' kumchagua Rais Mugabe wakati mpinzani wake ameshatangaza kujitoa kwa sababu zinazoeleweka; kuwa uchaguzi huo hautakuwa huru wala wa haki. Inaonyesha kuwa Mugabe anataka kufia madarakani. Lakini,yawezekana pia kuwa sasa amecheza karata yake ya mwisho na ameshindwa. Mugabe anakaribia kuondoka madarakani kwa aibu kubwa.Pichani ni miaka 21 iliyopita.Desemba, 1987.
Nimesimama Barabara ya Samora nikiwa na wana wawili wa mtalaamu wa Kitanzania aliyekuwa akilisaidia Shirika la Posta na Simu la nchi hiyo.Miaka 21 iliyopita niliiona Zimbabwe yenye umri wa miaka 7 tangu ipate uhuru.Kama ni mtoto,basi ulikuwa ni umri wa kwenda shule.
Nchi ilinawiri, dola moja ya Zimbabwe uliweza kuniwezesha kula mlo mmoja wa mchana na chenji ikabaki.(Leo Zimabwe imechapisha noti moja ya dola milioni kumi!)Nilifika Bulawayo nikaona dalili hizo hizo za matumaini.Nikaenda hadi vijijini sehemu za Mberengwa karibu na mpaka wa Msumbiji. Huko nikaona pia dalili za matumaini. Miaka kumi baadae, mwaka 1997 nikafika tena Zimbabwe.
Nikaanza kuona dalili za treni inayoacha njia. Niliyaona hayo Harare, Bulawayo na kule Nyanga, mbali sana na mjini. Ikawa ni tofauti kubwa na 1987 ambapo,nilizikuta shule za msingi zenye walimu bora, zahanati zilitoa huduma bora pia.Kwa mtazamo wangu,kinachomtokea Mugabe ni kile alichokipanda mwenyewe lakini anaogopa mavuno yake.Watoto wale niliowaona kule kijijini Mberengwa miaka 21 iliyopita ndio "Wanaomsumbua" Mugabe sasa.Wapepata elimu bora, sasa wanayaona mapungufu pia. wanataka kushiriki siasa za nchi yao kupitia vyama vingi.
Mugabe ameshindwa kusoma alama za nyakati. Wengi wa vijana wale aliowasomesha wakaja kuwa manesi bora barani Afrika, walimu bora pia. Wamekimbilia ughaibuni kwa vile Mugabe hawataki tena, kwa Mugabe hao "wameelimika sana!" Lakini, nao wanawaamsha wenzao walio nyumbani, vuguvugu la kutaka mabadiliko linaendelea. Miaka 21 imepita.Huu ni wakati wa Wazimbabwe kufanya mabadiliko hata kama ni kwa kumwaga damu.
Na ningependa nifike tena Zimbabwe, nione mwanzo mpya wa Zimbabwe.Na somo kubwa tunalojifunza hapa,ni namna gani mtu mmoja au kikundi cha watu kinavyoweza kuiingiza nchi shimoni kwa sababu za kifisadi.
Na
Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment