**AGNES MBAGA Mwalimu aliyepofuka baada ya
Ndoa..
Pichani ni Agnes Mbaga
---------------
KUNA methali nyingi za lugha ya Kiswahili, kati ya hizo ni ile inayotumiwa mara nyingi na Malenga wa utunzi wa mashairi inayosema ‘Hujafa Hujaumbika.’ Methali hii imezoeleka kutumiwa zaidi na watu wa mwambao wa pwani kuelezea maumbile ya mwanadamu yanavyoweza kubadilika wakati wowote akiwa hai, na kwamba, siku unapoaga dunia ndiyo inakuwa mwisho wa kuumbwa kwa mwanadamu.
Kuna mifano mingi kuthibitisha ukweli huu, wapo waliozaliwa na viungo vyote vya mwili lakini kutokana na sababu mbalimbali viungo vyao vimepungua au vipo wamekuwa walemavu. kwa mengi zaidi juu ya makala hii ya kusikitisha ya John Nditi fuatana nami nakupatia yote uone
KUNA methali nyingi za lugha ya Kiswahili, kati ya hizo ni ile inayotumiwa mara nyingi na Malenga wa utunzi wa mashairi inayosema ‘Hujafa Hujaumbika.’
Methali hii imezoeleka kutumiwa zaidi na watu wa mwambao wa pwani kuelezea maumbile ya mwanadamu yanavyoweza kubadilika wakati wowote akiwa hai, na kwamba, siku unapoaga dunia ndiyo inakuwa mwisho wa kuumbwa kwa mwanadamu.
Kuna mifano mingi kuthibitisha ukweli huu, wapo waliozaliwa na viungo vyote vya mwili lakini kutokana na sababu mbalimbali viungo vyao vimepungua au vipo wamekuwa walemavu.
Mwalimu Agnes Mbaga (32) ni miongoni mwa hao, alizaliwa akiwa na viungo vyote vya mwili, alisoma hadi chuo bila matatizo, lakini leo ana ulemavu wa kutoona.
Mwalimu Mbaga ana Stashahada ya Daraja A kutoka Chuo cha Ualimu Morogoro ambacho kinajulikana kwa jina maarufu ,Kigurunyembe, alikosoma mwaka 1995 hadi 1997, alipohitimu alipangiwa kufundisha Shule ya Msingi ya Rukose katika Tarafa ya Ngerengere wilayani Morogoro Vijijini.
“ Nilianza ajira yangu kwa mara ya kwanza katikati ya mwaka 1998 na ilipofikia Novemba mwaka huo niliugua homa kali ya uti wa mgongo …nilihangaikiwa sana nikitafutiwa matibabu na kwa nguvu za Bwana muumba wa yote niliweza kupona, lakini wakati huo tayari macho yangu yalikwishapoteza uwezo wa kuona tena, macho yangu yalikufa.
“Hii ilikuwa ni kuandika historia mbaya katika maisha yangu kutoka kwenye kuona na kuingia kwenye maisha ya upofu wa macho, nilifadhaika hasa siku za mwanzo wa maisha haya mapya” anasema.
Kwa mujibu wa Mwalimu Mbaga, wakati anasoma hadi kuhitimu elimu ya msingi, sekondari, Chuo cha Ualimu na hata wakati anaanza kazi ya kufundisha katika Shule ya Msingi Rukose hakuwa na matatizo ya macho, alikuwa na uwezo wa kuona kama mtu mwingine yeyote asiye na matatizo ya macho.
Hali ya kutoona ilifungua ukurasa mpya wa maisha yake, alianza kuishi bila kutoona, taratibu zake za maisha nyumbani na kazini zilibadilika.
Kutoona kulisababisha awe na wakati mgumu, ilibidi aikubali na kuizoea hali hiyo, ilibidi azoee kuishi na watu akiwaona lakini sasa ilimuwia vigumu kufanya hivyo.
“Baada ya kupata upofu huu nilikaa muda wa miaka mitatu bila kufanya lolote, nilishindwa kujihusisha wala kushiriki kazi za kijamii hadi mwaka 2001 nilipopata nuru mpya ya maisha,” anasema mwalimu Mbaga.
“Nilikata tamaa ya maisha kwa kuwa hali hii nilikuwa sijaizoea na ngeni katika maisha yangu mimi mbele ya wale niliokuwa nawahafamu …hili ndilo lililonifanya kukaa muda wote huo,” anasema.
Hata hivyo mwalimu Mbaga anasema mwezi Juni mwaka 2002 kwake ulikuwa ni mwezi wa ufunuo na mwanga mpya baada ya kupata mwaliko na Chama cha ‘TSB’( kinachohusika na walemavu wenye uono hafifu) na alihudhuria semina ya walimu wasioona wa Mikoa ya Dar es Salaam, Singida, Pwani, Dodoma na Morogoro ilifanyika Morogoro.
“Katika semina hiyo nilikutana na walimu wengi wenye ulemavu wa aina hiyo na nilianza kupata matumaini na kujiona kumbe naweza kuishi kama watu wengine kwa vile sikuwa peke yangu mwenye matatizo kama haya,” anasema mwalimu huyo.
Anasema katika semina hiyo, walimu wasioona waliandaliwa mafunzo katika stadi za ufundishaji na kuwajengea uwezo pamoja na matumaini katika shughuli hizo za kufundisha watoto wenye ulemavu wa kutoona na uono hafifu.
“ Kwa kweli hii semina ilinisaidia sana kwa kunipa matumaini mapya katika maisha yangu ya kila siku …niligundua kwamba kumbe wapo walimu wasioona na wanafanya kazi hii bila wasiwasi na wanao uwezo mkubwa wa kufundisha.
“ Hawa wenzangu walinitia moyo sana na kunipa mbinu za kufanya kazi katika mazingira haya na hii ilikuwa ni changamoto iliyonisaidia kunitoa hofu ya maisha yangu na kujiona sawa na watu wengine wa kawaida,” anasema.
Mwalimu huyo anasema baada ya kupata semina hiyo iliyomwondolea hofu, shughuli yake ya kwanza aliifanya baada ya kwenda Jijini Dar es Salaam kupata mafunzo mengine kwa walimu wasioona kwa mwaliko wa Chama cha TSB, mafunzo hayo ya pili yalimjengea uwezo zaidi katika kazi hiyo.
“Haya yalikuwa ni matunda mazuri kwangu, baada ya kumalizika kwa semina hii ya pili mwaka 2003 nilipelekwa kusoma katika Chuo cha Patandi kinachotoa mafunzo ya Walimu wa elimu maalumu ikiwamo ya watu wenye ulemavu wa macho na mwingine,” anasema.
Akiwa chuoni hapo aliweza kujifunza namna ya kufundisha wanafunzi kwa kutumia vifaa maalumu ikiwamo ile ya nukta nundu na stadi nyingine kuhusiana na masomo kwa watu wenye ulemavu na hatimaye kumaliza mwaka uliofuatia.
“Nilimaliza mafunzo yangu na kurejea mkoani Morogoro na kuomba uhamisho kutoka Shule ya Msingi ya Rukose na kuhamia Shule ya Msingi Mafiga ya Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu wa aina hiyo,” anasema Mbaga.
Anasema alianza kufundisha katika shule hiyo yenye kitengo cha elimu maalumu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kuona na wenye uono hafifu kuanzia Januari mwaka 2004.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, pamoja na kufundisha wanafunzi wenye ulemavu pia huwafundisha wanafunzi wanaoona.
Amesema, walimu wenye kuona huandaa mada za masomo husika, baadaye wanaziingiza katika mfumo wa maandishi maalumu ya wasioona na ndipo yeye huenda kufundisha.
“Vilevile wananisaidia kusahihisha madaftari ya wanafunzi wengine wenye uwezo wa kuona,” anasema.
Mwalimu Mbaga anasema anashukuru kuwa anafanya kazi zake kama wanavyofanya walimu wengine kwa sababu ya msaada wanaompa wa kumuandalia mada na kumsahihishia na hivyo imemsaidia kufundisha vizuri wanafunzi wa kawaida mara baada ya kumaliza kuwafundisha wenzao wenye ulemavu.
Anasema pia anaifurahia kazi yake ya ualimu pamoja na ulemavu alioupata. Mapenzi yake ya ualimu na kufundisha ndio yaliyompelekea kuwashawishi wazee wenye ulemavu wa kutoona kuanza kusoma na kuandika.
Mwalimu Mbaga anasema kuanzia mapema mwaka jana alianza kazi ya kufundisha darasa hilo kuanzia saa 10 za jioni kwa siku za Jumatatu na Alhamisi ya kila wiki.
“Ninafundisha darasa la jioni mara nikitoka shuleni kwangu Mafiga, nawafundisha wazee katika Shule ya Msingi Mwere ni la watu 15 kuanzia umri wa miaka 35 hadi 75,” anasema.
Akizungumzia changamoto anazozipata kwa wakati huu anasema ni ugumu wa kazi hiyo hasa kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi , umbali wa shule na ukosefu wa nyumba za kuishi walimu wenye matatizo kama yake.
Anasema anapokuwa shuleni huhitaji wasaidizi wa kike na wa kiume kwa ajili ya kuweza kumuongoza kwenda sehemu mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mbaga wasioona wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kushindwa kupigania usafiri wa daladala na wakati mwingine madereva hawawajali hasa wanapotaka kuvuka barabara pamoja na kwamba wanaonekana wakiwa na fimbo nyeupe maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kutoona.
Mwalimu Mbaga ni mke wa Boniface Mbugaje, walifunga ndoa Desemba 9, mwaka 1998 bado hawajabahatika kupata watoto.
Anasema, anaipenda ndoa yake na kumheshimu mume wake, katika siku za kazi, kila jioni humfuata kwa ajili ya kumchukua na kwenda wote nyumbani wanapoishi, Kihonda, Manispaa ya Morogoro.
Ulemavu huo haumzuii kufanya kazi za mikono nyumbani bila kuwa na msaidizi wa kazi.
Anasema wakati hajapatwa na matatizo hayo alikuwa ni mpenzi wa mchezo wa netiboli na alikuwa akicheza nafasi ya kati katika timu za shule ya msingi na sekondari , lakini kwa wakati huu mapenzi yake yamegeukia zaidi bustani za maua na kusali.
“Zamani nilikuwa mchezaji wa netiboli kabla ya kupatwa na janga hili, lakini sasa nimetokea kuyapenda sana maua ya asili na ya kawaida, kwani ishara ya upendo na amani…kwani yanaleta faraja,” anasema mwalimu.
Mwalimu Mbaga ni muumini wa dhehebu la Sabato, kila Jumamosi hupendelea kwenda kanisani kumwomba Mungu.
Huyo ndiye mwalimu Agness Mbaga ambaye amekataa upofu kuzimisha taaluma yake ya ualimu.
No comments:
Post a Comment