Tuesday, August 5, 2008

Shaggy Kuwasha Moto
Kwenye Tamasha la Zain
Bongo..
Meneja Masoko wa Kampuni ya Zain Tanzania,Costantine Magavilla(kulia)akizungumza na waandishi wa habari,Dar es Salaam jana kuhusu mwanamuziki mahiri kutoka Jamaica,Norville 'Shaggy'Rogers kuja nchini kutumbuiza mashabiki wa muziki katika tamasha litakalofanyika Ijumaa Agosti 8,mwaka huu,ikiwa ni moja ya matukio ya kusherehekea Celtel kutambulika kama Zain.Kushoto ni Meneja Uhusiano wa Zain Tanzania,Beatrice Mallya.
-------------
Zain Group,kampuni ya simu inayoongoza kwa kutoa huduma ya mawasiliano kwa zaidi ya wateja milioni 50 katika nchi 22 Mashariki ya Kati na Afrika,jana imetangaza tamasha litakalomshirikisha mwanamuziki mahiri kutoka Jamaica,Norville "Shaggy"Rogers kutumbuiza mashabiki wa muziki Tanzania,katika tamasha litakalofanyika Ijumaa Agosti 8,mwaka huu, ikiwa ni moja ya matukio ya kusherehekea Celtel kutambulika kama Zain.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Zain jijini Dar es Salaam,Meneja Masoko wa Zain Tanzania,Costantine Magavilla alisema mfalme wa Hip Hop Duniani na Dance Hall,Shaggy,anatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Alhamisi saa 12 jioni akiwa na wanamuziki wake 16 na atatumbuiza kwenye viwanja vya Leaders Club, tamasha linalotarajiwa kukonga nyoyo za mashabiki wengi wa Tanzania.Tamasha la Shaggy ni moja ya matukio mengi ambayo Zain imepanga kufanya katika kusherehekea kuzinduliwa kwa Zain Tanzania.

Wasanii wa Tanzania watakaopamba tamasha la Shaggy ni pamoja na Rashid Abdallah ‘Chid Benz’,Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’,Joseph Haule‘Profesa Jay’na makundi ya TMK Wanaume Halisi linaloongozwa na Juma Kassim‘Sir Nature’na TMK Wanaume Family chini ya Amani Temba‘Mheshimiwa Temba’.Wasanii wengine kutoka nje watakaotumbuiza katika tamasha hilo la Shaggy ni pamoja na Wahu na Nameless kutoka Kenya pamoja na kundi la Obsessions kutoka Uganda.
Zain Group itatoa tiketi 1,000 za bure kwa mashabiki wa muziki kutoka mtandao wowote watakaojibu maswali kuhusu Zain kwa usahihi kupitia vipindi vya radio.Pamoja na tiketi hizo Zain pia itatoa simu 30 kwa wateja wa Zain watakaojibu maswali hayo kuhusu Zain.Watanzania wengine watakuwa na fursa ya kununua tiketi kwa Tsh.7,000 na Tsh.10,000 katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Katika tamasha hilo la Shaggy,milango ya Leaders Club itafunguliwa kuanzia saa 10:30 alasiri na litaambatana na burudani mbalimbali kutoka kwa Ma-DJ watakaoonyesha vipaji vyao na pia wasanii kadhaa nchini wataanza kutumbuiza kuanzia saa 11 jioni.Magavilla alisema Zain inaona fahari kudhamini tamasha hilo ili kuwawezesha mashabiki wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla kupata burudani na kuwa miongoni mwa wanaosherehekea kuzinduliwa kwa Zain yenye kauli mbiu ya‘Wonderful World’(Ulimwengu Maridhawa).
“Zain kama mtandao uliosambaa sehemu mbalimbali duniani,inaamini huu ni mwanzo wa enzi mpya kwa wateja wa Zain Tanzania.Nembo mpya ya Zain ina rangi nyingi za kuvutia na imelenga kuhudumia wateja wa rika zote katika soko na tamasha hili ni sehemu ya shughuli za kusisimua tutakazoendelea kuwapa wateja wetu.

“Tunaamini wateja wetu wote na watu wengine Tanzania watajumuika nasi katika mabadiliko haya na kufurahia kauli mbiu yetu ya‘Wonderful World’inayowakilisha maisha mapya kwa wateja wetu,”alisema.Zain Group ilibadilisha jina katika nchi zote 14 ambazo inafanya shughuli zake barani Afrika kutoka Celtel na kuwa Zain,Agosti 1,2008,katika tukio la kihistoria lililojumuisha wafanyakazi,vyombo vya habari na watu mashuhuri.
Kama mtandao mmoja,Zain imejipanga vyema kutoa huduma nzuri kwa wateja wa Zain barani Afrika na Mashariki ya Kati.“Kwa kuibadilisha Celtel kuwa Zain,tunachukua mafanikio ya Afrika na kuyasambaza sehemu mbalimbali duniani,”alisema.Zain ni mtandao ulioenea katika nchi za Tanzania,Kenya,Uganda, Jamhuri ya Kongo,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Gabon, Zambia,Madagascar,Malawi,Niger,Nigeria, Sierra Leone,Burkina Faso na Chad.
Zain pia itazindua huduma zake nchini Ghana baadaye mwaka huu wa 2008.
Shaggy aliyezaliwa Orville Richard Burrell,Oktoba 22,1968,Kingston,Jamaica,albamu alizowahi kufyatua na kutamba ni pamoja na Hot Shot ya mwaka 2000 yenye nyimbo kama Not Fair, Leave It to Me,Freaky Girl.Albamu nyingine ni Boombastic(1995)yenye nyimbo za Forgive Them Father,Jenny,Heartbreak Suzie.

Pia alifyatua Clothes Drop(2005)yenye nyimbo za Would You Be,Ready Fi Di Ride,Luv Me Up, akatoa albamu ya Mr.Lover Lover:The Best of Shaggy,Vol.1 mwaka 2002 ikiwa na nyimbo kama Why You Treat Me So Bad,Big Up,Nice and Lovely na pia alifyatua albamu ya Hey Sexy Lady(CD/12")ya mwaka 2002 ikiwa na nyimbo kama It Wasn't Me(The Cartel Mix),Dance and Shout(Dance Hall Mix),Hey Sexy Lady.

Albamu nyimbo za Shaggy na miaka zilizotolewa na baadhi ya nyimbo kwenye mabano ni Lucky Day (2002)-Full Control, Strange Love,Shake Shake Shake,albamu ya Hot Shot(Germany Bonus Track)ya mwaka 2001 yenye nyimbo za Not Fair,Leave It to Me,It Wasn't Me.1999 alirekodi albamu ya Ultimate Shaggy Collection ikiwa na nyimbo za The Reggae Virus,Nice and Lovely,Why You Treat Me So Bad,mwaka 2002 akatoa albamu ya Hot Shot Ultramix yenye nyimbo za Keep'nIt Real(Swingers Mix),Dance and Shout(Dance Hall Mix),Freaky Girl (Strip Mix)na mwaka 2000 alifyatua Hot Shot Japan)ikiwa na nyimbo kama Not Fair,Leave It to Me na Freaky Girl.

No comments: