HABARI NJEMA...
Wanaoishi nyumba za NHC kuuziwa
-Kikwete
Wanaoishi nyumba za NHC kuuziwa
-Kikwete
---------------
Na Mgaya Kingoba,Iringa.
Sheria ya Mikopo ya Nyumba inatarajiwa kuwasilishwa bungeni Oktoba mwaka huu ambayo ikipitishwa, itawawezesha Watanzania wanaoishi kwenye nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kununua nyumba hizo,imefahamika. Rais Jakaya Kikwete alibainisha hayo jana mjini Iringa wakati alipozungumza kabla ya kuzindua maduka 74 ya wafanyabiashara yaliyojengwa na NHC katika eneo la Ipogoro katika Manispaa ya Iringa.
Rais Kikwete alisema maandalizi ya muswada huo yamekamilika na kwamba wiki ijayo yatafikishwa katika Baraza la Mawaziri kwa uamuzi wa mwisho, kabla ya kupelekwa kwa wanasheria ili kuandaa muswada wa kupelekwa bungeni Oktoba mwaka huu.“Tunaandaa Sheria ya Mikopo ya Nyumba (mortgage financial),ambayo itamwezesha mtu anayekaa katika jengo la flat(ghorofa) za NHC akapata hati,nyumba ikawa yake na kuwa na dhamana ya kukopa,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na wananchi.
“Hii iko katika hatua za mwisho, mapendekezo yote yamekamilika na wiki ijayo yatafikishwa katika Baraza la Mawaziri na kisha kupelekwa kwa wanasheria ili kuandaa muswada wa kupeleka bungeni,”alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa baada ya Bunge kupitisha sheria hiyo,ataisaini haraka ili ianze kazi kwa sababu itakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania. Alisema mtu hawezi kuishi ndani ya nyumba ya NHC kwa miaka 30 bila kufaidika,huku shirika hilo likijenga nyumba zaidi kutokana na kodi za wapangaji hao.
“Ili mpangaji kununua nyumba ni lazima apate hati, hivyo ukinunua flat za NHC zitakuwa mali yako,NHC watabaki na umiliki wa kiwanja.Nyumba itakuwa yako wewe, hakutakuwa na ugomvi na NHC,isipokuwa utabaki ugomvi wenu wapangaji kuhusu kufagia ngazi;mara mwenzetu anafagia anaacha taka kwenye ngazi,”alisema.Aidha,alisema sheria nyingine itakayopelekwa bungeni itaiwezesha NHC kukopa fedha za kujenga nyumba nyingine kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha.
“Serikali haiwezi kutoa fedha kwenu kwa sababu wakati mwingine inakuwa tabu; huku ukiwa na majukumu ya kusaidia elimu,hospitali na barabara. Lakini tunachoweza kufanya ni kuweka utaratibu wa kupata fedha za mkopo,”alisema. Alisema sheria hizo zote mbili zitakuwa na manufaa kwa sababu wananchi watapata fursa ya kujenga kwa kutumia mikopo hiyo na kulipa polepole huku NHC nayo ikikopa na kujenga nyumba nyingine;lakini akawapa changamoto ya kuuza baadhi ya majengo na kujenga mengine wakati sheria hiyo itakapoanza kazi.
Awali, akitoa maelezo ya mradi huo wa maduka ya Ipogoro,Mkurugenzi Mkuu wa NHC,Martin Madekwe,alisema kwa kuangalia uwezo wa kifedha,ni dhahiri shirika hilo halitaweza kukidhi maombi mengi ya kujenga kutoka mikoa na wilaya mbalimbali.Labda kwa msaada wa serikali tu, kwa maana ya ruzuku ndipo shirika litaweza kutekeleza maombi haya mengi.Njia nyingine ni pale mfumo rasmi wa kutoa mikopo kwa riba nafuu na kupata soko imara la kuuza nyumba chache inayojenga,”alisema Madekwe.
No comments:
Post a Comment