Tuesday, June 17, 2008

Usafiri wa vipanya kupigwa marufuku Dar ifikapo Agosti
*Daladala sasa kujisajili kwenye kampuni*

Hussein Issa na Martha Ndeki

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini, (Sumatra), imesema daladala aina ya Hiace, maarufu kama 'vipanya', hazitaruhusiwa kutoa huduma ya kusafirisha abiria jijini Dar es Salaam, ifikapo Agosti Mosi, mwaka huu.

Badala yake, Sumatra imesema huduma hiyo itatolewa na magari makubwa yenye uwezo wa kuchukua abiria zaidi ya 25, badala ya 'vipanya', ambavyo vina uwezo wa kubeba abiria 18 tu walioketi.

Hata hivyo, Sumatra imesema magari yatakayoruhusiwa kutoa huduma hiyo, lazima yawe ni mapya na yasiwe yametumika zaidi ya miaka mitano, kama inavyofanyika hivi sasa.

Mkurugezi Mkuu wa Sumatra, Israel Sekirasa alisema uamuzi huo unatokana na kanuni mpya za viwango vya magari ya usafiri wa umma, ambayo inazuia magari yenye uwezo wa kuketisha abiria chini ya 25 kutoa huduma za usafiri huo mijini.

Sekirasa alisema hayo kwenye mkutano wa wadau wa kukusanya maoni, kuhusu maombi ya wamiliki wa mabasi ya kuongeza gharama za usafiri Dar es Salaam, uliofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini.

''Kwa mujibu wa kanuni mpya za viwango vya magari ya usafiri wa umma, magari yenye uwezo wa kuketisha abiria chini ya 25 hayafai kutoa huduma za usafiri wa umma,'' alisema Sekirasa.

Kutokana na hali hiyo, alisema Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), imeombwa kusitisha kuandikisha magari hayo kuanzia tarehe hiyo, ili kutowapa hasara watu wote ambao wameshaagiza magari au wako katika utaratibu wa kuyaandikisha.

Alilitaka Shirika la Viwango nchini (TBS) na TRA, kutokubali uingizwaji wa magari yanayokusudiwa kufanya biashara ya abiria ya kawaida, kukodisha kwa ajili ya shughuli za kitalii au makundi maalum, ambayo si mapya na yote yanayozidi miaka mitano.

''Inatarajiwa kwamba kuanzia tarehe 1/9/2008, ni magari mapya tu au yale yasiyozidi miaka mitano ndiyo yatakayokuwa yanapitishwa na TBS na kusajliwa na TRA,'' alisema Sekirasa.

Alisema magari mengi nchini, hivi sasa yanatumika kwa zaidi ya miaka 18, badala ya miaka saba au nane kama ilivyo katika nchi zilizoendelea.

''Gari likishatumika zaidi ya miaka mitano baada ya kusajiliwa, halitaruhusiwa kubeba abiria kwani litakuwa limeshachakaa,'' alisema Sekirasa.

Aliwahimiza wamiliki kuunganisha nguvu na kuanzisha makampuni ya usafirishaji.

Pia, aliiagiza TRA na TBS kutoruhusu uingizaji wa magari ya abiria nchini, ambayo yametumika kwa muda wa miaka mitano pamoja na kutoyapatia leseni.

Alisema kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu magari yasiozidi 500 ndiyo yatakayokuwa yamepitishwa na TBS na kusajiliwa na TRA.

Mkurugenzi Mkuu huyo, aliwataka wamiliki wa vyombo vya usafirishaji nchini kuleta mabadiliko katika usafiri mijini.

Alisema mamlaka haitatoa leseni kwa mmiliki mmoja mmoja, bali itakuwa inatoa kwa makampuni, au makundi ya watu watakaokuwa wamejiunga kwa pamoja, kwa lengo la kuleta ushindani wa usafirishaji nchini.

�Tunatoa rasmi taarifa kuwa tunatarajia kutoa leseni ya usafirishaji kwa makampuni badala ya mtu mmoja mmoja,� alisema Sekirasa na kuongeza:

''Ni vyema wamiliki wakaanza kujipanga, kuanzia sasa kwa kuanzisha makampuni yatakayoweza kumiliki magari mapya ya kisasa ili kuweza kufaidika na uwekezaji unaoendelea''.

Alisema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, inaandaa mipaka ya eneo la kati la jiji na kwamba, baada ya kutangazwa, hakuna "kipanya" kitakachoonekana katika eneo hilo.

''Ofisi yangu kwa kushirikiana na halmashauri ya jiji na DART (Mamlaka ya Leseni Mkoa wa Dar es Salaam), tutapanga njia upya kuzingatia hili,'' alisema Sekirasa.

Akizungumzia mradi wa mabasi yaendayo kasi, alisema wanatarajia kuwa utakuwa umekamilika na huduma kuanza kutolewa ifikapo mwaka 2010.

"Itakuwa rahisi kupitia makampuni kuweza kuingizwa katika mfumo wa kisasa wa usafiri, ili kuweza kutoa huduma katika njia zitakazojaza njia kuu za mradi," alisema Sekirasa.

Aliwataka wamiliki kuanzisha makampuni yatakayoweza kumiliki magari mapya ya kisasa, ili kuweza kufaidika na uwekezaji unaoendelea.

Sekirasa alisema wasafirishaji wengi wamekuwa wakiagiza magari yaliyotumika ambayo licha ya kuchafua mazingira, gharama zake za uendeshaji ni kubwa na kusababisha ongezeko la gharama za uendeshaji kuakisiwa katika nauli zinazotozwa na wasafirishaji hao.

Akichangia suala hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Wamikili wa Magari ya Abiria Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk, alipendekeza nauli iongezeke kwa asilimia 35 kwa kituo.

Alisema hana pingamizi na uamuzi huo wa kuzuiwa vipanya kutoa huduma, lakini alisisitiza maombi yao ya kutaka ongezekezo la nauli ya daladala yakubaliwe.

Alionyesha masikitiko yake kwa serikali kutangaza msamaha wa kodi ya magari, huku magari ya abiria yakinyimwa msamaha huo, badala yake ukaelekezwa kwenye malori, ambayo kazi yake ni kupakia mizigo na michanga pekee.

Kuhusu wanafunzi, alitaka nauli zao ziongezeke kwa kutozwa nusu ya nauli ya mtu mzima kwa vile askari wa majeshi hawalipi kabisa nauli.

Meneja wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), Peter Sangu alisema kutokana na kupanda kwa bei za mafuta, shirika lake linapendekeza nauli iongezeke kwa asilimia 40 kwa kituo.

Madereva na makondakta wa daldala walimweleza mwandishi wa habari kuwa hili likielekezwa watageuka kuwa vibaka (wezi) kwa sababu ajira zao zitaisha.

Dereva wa daladala linalotoa huduma kati ya Mwenge na Temeke, Daudi John alisema uamuzi wa kuzuia 'vipanya' kutoa huduma, utasababisha madereva wafanye kazi ya wizi, kwa sababu wengi wao watapoteza ajira.

''Wengi tunatafuta maisha katika haya haya magari mwana, hivyo, wakiyafutia leseni tena noma,'' alisema Daudi.

Naye Juma Masoud, anayeendesha daladala kati ya Ubungo na Buguruni, alisema endapo magari hayo yatazuiwa kutoa huduma, abiria watapata tabu ya usafiri.

Alisema hajafurahishwa na uamuzi huo, kwa vile ni mpya, magari makubwa ni machache na kwamba, yote yatakayokuja, yatakuwa ni ya wakubwa ambao wana madereva wao.

jamani hii imekaaje maana kuhusu swala la kutoa vipanya nimelisikia tangu nikiwa secondary ila hii kweli itasaidia au ndio kama kawa kukurupuka tu kwa nini nasema ni kukurupuka maana kwa sasa tu usafiri hautoshelezi jijini na hayo mabasi watayashusha mangapi maana haya mambo yakufanya bila kufikiri sio mambo kabisa sasa na hao wamiliki wa hivyo vipanya itakuwaje na hao madereva na makonda wao mmewaandalia ajira gani au ndio hayo magari mtakayo leta mtawapa madereva wa vipanya na pia kusema hamtasajili kwa mtu mmoja moja kama sasa ndio kuwafanya hata wale walio na uwezo wakununu magari japo moja wasiweze kwa kikwazo chenu cha kujisajili kama kampuni jamani naomba muangalie sio kuongea bila kuangalia pande zote hizo nawatakia kila la kheri maana sisi tupo kwa ajili ya kukosoa na kusifia kwa yale mnayo yafanya kama Mwaibula alitubunia maswala ya mistari wakati huo katika magari na pia kwa yale mambo korofi ya kuhakikisha magari ya abiria yanamalizia safari zao yameisha wapi maana hatuoni hata mabadiliko !! wadau mchangie

No comments: