NI kweli inawezekana uko katika hali fulani ngumu katika maisha, lakini nina hakika na ndio ukweli wenyewe kwamba ukiwa makini na kutafakari kwa makini ulikotoka, uliko na kule unakoelekea, unaweza kufanikiwa mipango yako.
Kama nilivyoeleza katika makala iliopita, maisha ni kama vita, ili ushinde ni lazima ujue jinsi ya kupigana, wala usitegemee yuko mtu hapa duniani kwa ajili ya kukusaidia katika maisha yako ili uwe na mafanikio.
Utashiba kwa kazi za mikono yako. Zingatia hilo, hii ina maana kuwa unapaswa kuongeza jitihada kwa kila unachofanya ili uwe mwenye mafanikio maishani mwako; kama ni kusoma, soma zaidi, kama ni kazi ifanye zaidi, kama ni shughuli nyingine yoyote, ifanye kwa ufasaha.
Ndugu zangu kuna misemo mingi tumekuwa tukiisikia mitaani, mingi haina maana, hiyo ndio sababu nimeona leo niwaletee misemo yenye akili, kiasi kwamba hata unapoizungumza mbele za watu, watakuona ni mwenye hekima na zaidi ya yote ukiipendelea kuizungumza na kuifanyia kazi, maisha yako yanaweza kubadilika sana, ukawa mwenye ujasili, mwenye mafanikio nk.
Malengo ni ndoto yenye ukomo (A goal is a dream with a deadline)
Ni kwamba kama unaweka malengo kwamba nataka kufanya hili na lile, ni lazima liwekee ukomo kwamba kwa mfano ifikapo Juni, lazima niwe nimenunua gari nk. Malengo bila kuweka ukomo ni sawa na bure.
Utajua kama una akili au la kulingana na maisha uliyonayo Hapa nazungumzia jinsi ya kujipima akili (intelligence test); Jinsi unavyoishi ni matokeo ya matendo yako, lakini pia hata utakavyokuwa kesho ni matokeo yako.
Acha kulaumu wengine, wala usilaumu kwanini labda umezaliwa kwenye familia maskini, kuna watu wengi wametokea familia maskini kisha wakawa watu wakubwa baadaye, kati yao ni Patrice Lumumba, Waziri Mkuu wa zamani wa Congo (DRC), Julius Nyerere na wengine wengi.
Lawama sio tiba ya matatizo yako
Unapokuwa na tatizo usipoteze muda kujilaumu, badala yake tafuta njia za kuondokana na tatizo hilo. Unapolaumu, hutafuti suluhu, bali unajiongezea mzigo mwingine wa mawazo...jisemee "Nimekosea hili na nimepata matatizo, lakini cha kufanya ni hiki na kile".
Mawazo mema huzaa mema
Wote walio matajiri, wanaofaulu mitihani, kuwa maarufu nk walikuwa na mawazo yaliyowafikisha huko. Aidha katika maisha ni vizuri kuachana na maneno au mawazo ya laana...maana utakuta wengine wanajilaana wenyewe kwa kusema kwa mfano "Mimi mtu wa kutoka familia maskini bwana siwezi kuwa na maisha mazuri"...
Nani kakwambia huwezi kuwa tajiri, nani kakwambia huwezi kufaulu vizuri masomo eti kwa sababu kwenu hakuna umeme...mbona wengi tu wamesomea vibatari usiku na wakafaulu vizuri...Acha kuweka visingizio, pigania ushindi katika maisha kulingana na hali uliyonayo.
Unasubiri hadi uwe na mazingira mazuri ndio ufanye jambo fulani, hilo zuri utapata lini? Wengine eti anasubiri apate fedha nyingi ndipo ajenge nyumba nzuri, ndipo anunue gari zuri, hiyo si sahihi, fanya mambo kulingana na uwezo uliopo.
Pendelea kuwaza mazuri zaidi
Kadri unavyowaza mazuri mara kwa mara, ndipo unapotengeneza maisha yako kuwa mazuri. Waza mambo makubwa, badala ya kufikiria kwa mfano kuanzisha mradi wa kuuza karanga, waza kuuza magari...hata kama huna fedha elewa kuwa watu nje ya nchi wanatafuta watu wa kuwauzia vitu hapa nchini, waweza kuwa wakala wao, cha msingi ni kujieleza vizuri na kuwa mwaminifu.
Kumbuka hakuna ushindi bila malengo...nini maana ya malengo?...tumeshaona juu kwamba ni mipango yenye deadline (ukomo).
Kabla ya kupata ushindi, tegemea upinzani
Kabla ya kufanikiwa katika jambo zuri, mara nyingi huwa lina upinzani, pia wapo wengine watakukatisha tamaa kwamba aaah bwana kashindwa fulani tena alikuwa ana fedha na elimu ya kutosha, utaweza wewe bwana...siku zote huwa siwapendi watu wenye midomo kama hii, nataka mtu ambaye ananitia moyo, yeyote mwenye kukatisha tamaa, usipendelee kumsikiliza, kama ni rafiki jiepushe naye.
Penda mtu ambaye anakutia moyo, anakuonyesha njia, hata kama somo ni gumu kiasi gani, badala ya kusema huwezi, anakwambia aaah kama mwalimu huyu hafundishi vizuri, hebu twende kwa mwalimu mwingine hata kama ni shule jirani. Katika maisha kila jambo linawezekana.
Makala nyingine wiki jumamosi ijayo usikose uangalia mtandao wetu huu !
No comments:
Post a Comment