Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala Jijini, Bw. Mohamed Yakub, amesema mikakati ya kudhibiti ukimwi isipowekwa na kuwashirikisha wadau wa kupambana na ugonjwa huo jamii itazidi kupoteza watu na idadi ya yatima kuongezeka.
Ameyasema hayo wakati akifungua warsha ya wadau wa Ukimwi inayojadili maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani jijini, inayoadhimishwa kila mwaka Desemba mosi.
Meya Yakub alisema kuwa wadau wanayo fursa ya kuweka mikakati itakayowezesha kufanikisha siku hiyo kwa kutoa mawazo na michango ya jinsi watakavyoiadhimisha ikiwemo, kuendesha zoezi la upimaji wa Ukimwi kwa hiari
Warsha hiyo inayo nafasi ya kujadili namna ya kuandaa mazingira bora kwa ajili ya ustawi wa yatima ambao wamekuwa wakiongezeka kila siku kutokana na maradhi hayo.
”Mkoa wa Dar es Salaam unashika nafasi ya tatu kwa kuwa na asilimia 10.6 ya maambukizi ya virusi vya ukimwi kwakweli hali ni mbaya. Lazima tuhakikishe kuwa tuna mikakati madhubuti ya kupunguza ongezeko hili,” akasema Bw. Yakub.
Akasema mkoa wa Iringa unaongoza kwa kuwa na maambukizo kwa asilimia 13.5, ukifuatiwa na Mbeya wenye asilimia 13.4.
Mratibu wa Ukimwi wa Manispaa ya Ilala, Bi. Elina Nachibona, amesema maadhimisho hayo Jijini yatafanyika katika manispaa yake kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kutokana na ukweli kuwa kampeni za hiari za upimaji wa virusi zilizinduliwa hapo na Rais Jakaya Kikwete mnamo mwezi Julai 14 mwaka huu.
Akasema siku hiyo tathmini ya kampeni hiyo itafaanyika na wananchi wataendelea kuhamasishwa kupima afya zao kwani Tanzania bila Ukimwi inawezekana.
Akasema yatakuwepo maonyesho kutoka watu na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na mapambano dhidi ya ugonjwa huo pamoja na kutoa elimu.
No comments:
Post a Comment