Mufti Mkuu Simba apangua
Bakwata..
SIKU moja baada ya Mufti Mkuu wa Tanzania, Shekhe Issa Shaabani Simba(Pichani) kuingia katika ofisi yake tangu alipotoka nchini India kwa matibabu, ameung'oa uongozi wote wa juu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzani (BAKWATA) kuanzia na aliyekuwa Naibu Mufti, Shekhe Abubakar Zubeir. Kwa mujibu wa taarifa ya BAKWATA iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana usiku na kusainiwa Mufti Simba,Alhaj Shekhe Suleiman Mohamed Gorogosi ameteuliwa rasmi kuwa Naibu Mufti mpya.
"Nimebatilisha na kutengua uteuzi wa Shekhe Abubakari Zuberi kuwa na Naibu Mufti na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa. Kwa mantiki hiyo sasa Shekhe Gorogosi ndio anashikilia nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Shekhe Zuberi," alisema Mufti Simba katika taarifa yake. Katika mabadiliko hayo pia Mufti Simba amevunja kamati ya hijja ya BAKWATA Makao Makuu na kuhamishia shughuli zote za hijja chini ya Ofisi ya Naibu Mufti Mkuu Dini BAKWATA Taifa.
Pia amemteua Ustadhi Mohamed Hamis Said kuwa Katibu wa Baraza la Ulamaa, kutengua uteuzi wa Shekh Hamisi Mataka kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya BAKWATA Taifa na kulipanga upya Baraza la Ulamaa na kuwateua wajumbe wa baraza hilo.Kwa mujibu wa taarifa hiyo wajumbe wapya wa baraza hilo ni Alhaj Shekhe Tawfiq Ibrahim Malilo ambaye ni Shekhe Mkuu Mkoa wa Kigoma na Shekhe Mhamed Mkanga ambaye ni Shekhe Mkuu Mkoa wa Tanga.
Wengine ni walioteuliwa katika baraza hilo ni Shekhe Suleiman Mohamed Gorogosi ambaye ni Shekhe Mkuu Mkoa wa Lindi, Shekhe Ismail Habibu ambaye ni Shekhe Mkuu Mkoa wa Shinyanga na Shekhe Salum Fereji ambaye ni Shekhe Mkuu Mkoa wa Mwanza.
"Nimeamua kulipanga upya BAKWATA na nimeagiza mabadiliko hayo kuanza kazi mara moja. Nimetoa nakala ya mabadiliko haya kwa mashekhe wa mikoa yote Tanzania, Wenyeviti wa BAKWATA wa mikoa na makatibu wa Mikoa Tanzania," alisema Mufti Simba. Habari hii na Said Mwishehe
No comments:
Post a Comment