Wednesday, June 4, 2008

Mgodi wa Kiwira si wa Mkapa-Tabaro


Uongozi wa Kampuni ya Kiwira Coal and Power Ltd (KCP) inayomiliki mgodi wa Kiwira, umekanusha madai kuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe Anna ni miongoni mwa wamiliki wa mgodi huo.
Badala yake, huo umesema Kampuni ya ANBEN inayomilikiwa na Mkapa na mkewe, ambayo awali ilikuwa sehemu ya Kampuni ya Tanpower, ilijitoa baada ya baadhi ya wanahisa wenzake kuwa na mpango wa kununua mgodi huo. Mtendaji Mkuu wa KCP,Francis Tabaro, alisema ingawa katika hati za umiliki (Articles of Association) inaonyesha kuwa Mkapa ni sehemu ya Tanpower, lakini baadaye alijitoa.


“Ni kweli ANBEN ilikuwa sehemu ya Tanpower lakini baada ya wazo la kununua Kiwira kuingizwa na wadau wenzake, yeye aligoma akaona aitoe kampuni yake katika Tanpower,” alisema Tabaro. Tabaro pia alikanusha madai kuwa Anna Mkapa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwira na akaeleza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote, kwani kampuni hiyo haihusiani na kiongozi huyo.


Tabaro aliwataja wakurugenzi wa KCP kuwa ni Joseph Mbuna ambaye ni Mwenyekiti, Mafuru M. Mafuru, Wilfred Malkia na Evans Mapundi wakati serikali yenye hisa 15 katika mgodi huo inawakilishwa na Omari Chambo ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Asumpta Ndimbo.
Tabaro alisema upotoshaji unaofanywa na vyombo vya habari kuwa Rais mstaafu Mkapa ni sehemu ya wamiliki wa mgodi huo, hazina ukweli, bali zinalenga kuharibu jina la kampuni ambayo imechukua hatua ya kuendesha mgodi huo. “Mkapa, mkewe au familia yake si sehemu ya wamiliki wa mgodi huu,” alisisitiza huku akionyesha kukerwa na namna alivyodai kuna upotoshaji wa makusudi unaofanywa na vyombo vya habari.
Alisema lengo la kuripoti habari hizo ni kutaka serikali iwe na mtazamo hasi juu ya mgodi huo, hali ambayo inaweza kuzorotesha uzalishaji wa makaa ya mawe. Tabaro pia alisema kitendo cha baadhi ya maofisa wa serikali kutoa maelezo kuwa mgodi huo unachunguzwa kuhusiana na madai kuwa ulichukuliwa isivyo halali na Kampuni ya KCP, kunaweza kukaifanya kampuni hiyo kushindwa kupata fedha za kuendesha mradi huo.Habari hii na Mwandishi Maalum TSN

No comments: