
Richard Bezuidenhout (pichani) ni miongoni mwa majaji wa kinyang`anyiro cha kumtafuta mrembo wa Tanzania Uingereza “Miss Tanzania Uk 2008” itakayofanyika Jumamosi hii katika ukumbi wa Silverspoon Banqueting hall uliopo Wembley.
Hayo yamethibitishwa leo na Mwenyekiti wa kamati ya Miss Tanzania Uk, Bw. Juma Mabakila ambae alisema mbali ya kuwa jaji, Richard pia atapata nafasi ya kuwashukuru Watanzania wa Uingereza kwa mchango wao mkubwa waliotoa wakati alipokuwa katika jumba la Big Brother Afrika mwaka jana kule Afrika Kusini.
Mabakila alisema Richard atapata nafasi kutembelea sehemu mbalimbali ikiwemo kuona uwezekano wa kuwa mgeni mwalikwa katika jumba la Big Brother Uk iliyoanza wiki iliyopita na kupata nafasi ya kumtembelea ofisini balozi wa Tanzania Uingereza, Mwanaid Senare Maajar.
Mbali na Richard, Mabakila alisema majaji wengine ni mwenyekiti wa kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga na Jacquline Berand Mafuru ambae alishawahi kushiriki mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2003.
Richard baada ya kuishi pamoja ndani ya nyumba ya Big Brother II kwa siku 98, aliweza kuibuka kidedea kwa kujinyakulia dola laki moja akifwatiwa na Ofuneka (Nigeria) na mshindi wa tatu ni Tatiana (Angola).
Richard alichaguliwa na nchi 7, ofuneka nchi 5 na Tatiana mshindi wa tatu nchi 1 tu kwenye fainali iliyofanyika Novemba 11 mwaka jana Johannesburg,Afrika Kusini.
Akiwa katika jumba hilo alijikuta akitumbukia katika dimbwi la mapenzi, kwani alikuwa mshiriki pekee aliyeweka rekodi ya kupigiwa kura ya mapendekezo atoke mara nyingi zaidi. Kwani mara zote tano alizopigiwa kura aliweza kunusurika, hivyo kusafishiwa njia ya kujitwalia kitita cha dola 100,000 (zaidi ya Sh. milioni 130).
No comments:
Post a Comment