Thursday, August 14, 2008

libeneke la madenti urusi
picha zikionesha wanafunzi wanaosoma urusi wakiwa ubalozini moscow




UKWELI ULIOSABABISHA VIJANA WA MWAKA WA LUGHA(2007-2008) CHUO KIKUU CHA URAFIKI LUMUMBA NCHINI URUSI KUWASILISHA KILIO CHAO UBALOZINI KWA MUDA WA SIKU NNE MFULULIZO. KAMA INAVYOELEZWA NA MWENYEKITI WA UMOJA WA WANAFUNZI HAO
Mimi, mwenyekiti wa umoja wa wanafunzi wa kitanzania wapatao 148 wanaosoma Chuo Kikuu cha Urafiki (Lumumba )nchini Urusi, nimesikitishwa sana na hatua ya ubalozi wetu pamoja na wizara yetu ya elimu kuamua kuubadilisha ukweli ili waweze kufanikisha matakwa yao.

Ninasema hivyo kutokana na ukweli kuwa mimi pamoja na wenzangu tuliomaliza mwaka wa pili tuliletwa kwa mkataba huo huo ulio waleta vijana hawa. Matatizo haya yanayo wapata vijana hawa wa mwaka wa maandalizi ya lugha hata sisi yalitupata miaka miwili iliyopita, kwani tulifika Urusi tarehe 31/11/2005 badala ya tarehe 1/9/2005, hii ikimaanisha kuwa tulichelewa miezi mitatu.
Hali hii ya ucheleweshwaji wa wanafunzi kufika urusi huchangia matatizo mengi sana mojawapo ikiwa ni baadhi ya wanafunzi kurudia mwaka wa masomo kutokana na kucheleweshwa kufika nchini urusi, kwa mujibu wa wizara ya elimu tulipaswa kulipwa fedha za miezi tisa,wakati huo balozi wetu aliyekuwepo Patrick Chokala alidai kuwa fedha za mwezi wa kumi na moja 2005 alituombea kwa serikali kama huruma tu ingawa ilikuwa ni haki yetu.

Mimi niliyekuwa katibu mkuu wa umoja wa wanafunzi wa kitanzania chuoni kwetu wakati huo,pamoja na viongozi wenzangu hatukukubaliana na swala hilo kwani kwa utaratibu wa serikali yetu (wizara-bodi ya mikopo), mwanachuo hulipwa fedha kulingana na mwaka wa masomo yaani (September-august) kila mwaka, pia ukizingatia kuwa wakati tunakuja Urusi tulisaini fomu za mikopo kwa ajili ya mwaka mzima wa masomo, kitu kingine kinachoonyesha ukweli huo ni kuwa pamoja na kuchelewa kufika chuoni, serikali yetu hulipa ada zetu za kozi ya lugha kwa kipindi cha mwaka mzima ,sio hilo tu ila hata bima ya afya serikali yetu hulipa na inaendelea kulipa kuanzia(septemba-august).

Vile vile wakati matokeo yanatoka kwamba tumechaguliwa kuja kusoma urusi kuna wengine kati yetu walikuwa wameanza masomo katika vyuo vikuu mbali mbali nchini, lakini baadaye wakapata nafasi ya kuja kusoma urusi hali hiyo ilipelekea wanachuo hao kuandika barua ya kuomba mikopo yao kuhamishiwa Urusi kama walivyo agizwa na wizara kuandika barua hizo, na walitekeleza agizo hilo la wizara.

Hivyo basi wizara iliwahakikishia wanachuo hao kupata fedha zao za mwaka wa masomo(2007-2008) watakapofika nchini urusi. Ukizingatia hayo yote pamoja na ukweli kuwa mwanafunzi anayekuja kusoma Urusi ni mgeni wa mazingira ya urusi na anakuja kuanza maisha upya, hii ikiandamana na gharama za lazima za awali ambazo wizara yetu ya elimu pamoja na ubalozi wetu hautaki kuzikubali mfano nguo za baridi kwani ukicheza na baridi ya Urusi unaweza kuathirika kiafya.

Vilevile tunahitaji viatu vya kujikinga na baridi, pamoja na vyombo vya kutuwezesha kujipikia wenyewe kwani wanafunzi walio wengi huwalazimu kujipikia wenyewe kutokana na ukweli kuwa, kiwango cha fedha za kujikimu kinachotolewa na serikali yetu humwezesha tu mwanafunzi kujipikia mwenyewe kwani ukila katika migahawa ,kiasi hicho cha fedha hakiwezi kukufikisha hata nusu ya mwezi.
Kutokana na sababu hizo nilizozitoa za msingi tuliamua mwaka 2006 kuzifuatilia fedha za miezi miwili yaani (September na Oktober) ambayo hatukupewa kwa madai kuwa hatukuwa tumefika Urusi, lakini kila tulipowasiliana na ubalozi tulipigwa danadana mpaka tukakata tamaa lakini tulijitahidi kuwaonyesha na kuwaelezea sababu za msingi kuwa fedha hizo zilikuwa ni halali yetu na haki yetu pamoja na hayo waliendelea kushikilia msimamo wao, cha ajabu tulipokaribia kumaliza mwaka wa lugha tulipewa kwa ghafla fedha hizo na tulipohitaji maelezo tuliambiwa tusiulize zitokako, pamoja na hilo tulielewa ni zile zile tulizokuwa tukizidai.

Sasa ndugu zangu watanzania naomba niwahakikishie kuwa huo mkataba uliotuleta sisi 2005 ndio uliwaleta ndugu zetu 2007 katika chuo hicho hicho, na hawa nduguzetu ndio leo wapo katika maisha magumu na yakukatisha tamaa, kufuatia ukweli kwamba walipewa fedha za miezi kumi na moja tu (September 2007-July 2008) badala ya miezi kumi na miwili, yaani mwaka mzima wa masomo (September 2007-August 2008).

Mimi kama rais wa umoja wa wanafunzi hao, nimejaribu pamoja na viongozi wenzangu kuwasilisha matatizo haya pamoja na mengine mengi , yakiwemo ya fedha za malazi, fedha za mafunzo kwa vitendo (practicals), fedha za vifaa vya shule (stationeries) pamoja na fedha za madawa ubalozini, lakini hakukuwa na majibu yoyote ya kuridhisha,kutokana na hilo na ukweli kuwa vijana waliishiwa fedha kutokana na ugumu wa maisha waliamua kupiga hodi ubalozini ili kujua mustakabali wao kwani walishindwa kuishi bila fedha hizo ambazo wanaamini kivyovyote ni haki yao kama ilivyo kuwa haki yetu 2006, kwani naamini isingelikuwa ni haki yetu mwaka 2006 tusingelipwa fedha hizo, kumbukeni kuwa maisha ya Moscow yamepanda kuliko kawaida (Moscow ni mji wa kwanza wenye maisha ghali duniani), sasa kwanini ukweli huu unabatilishwa?

Niukweli kuwa vijana hawa wanaosoma mwaka wa lugha 2007-2008 wanastahili malipo haya. Kama mlivyosikia sikuzote ukweli kuwa Urusi ni nchi ambayo kazi kwa wasio raia wa Urusi kupatikana ni ndoto na ukibahatika kuzipata japo za kuosha vyombo ukitoka au ukienda kazini unarudi hostel na manundu kwani skin haters (wabaguzi wa rangi) wakikupata amazako ama zao.

Ninaamini kabisa kuwa serikali yetu inamalengo mazuri kabisa na sisi lakini kuna watendaji wachache Serikalini, wanaojaribu kuupindisha ukweli na kuipaka matope Serikali kwa manufaa yao binafsi. Naomba tuondoe ubinafsi kwani itakuwa hasara kwa taifa langu nikifa kwasababu nilikuwa natafuta fedha za kujikimu.
Kwa kuwa Serikali yetu ilituleta Urusi kusoma na kupata ujuzi ili tukalitumikie Taifa letu, basi ninaomba ituhudumie ili tumalize masomo yetu na turudi nyumbani salama.
Ninamnukuu aliyekuwa balozi wetu Patrick chokala mwaka 2006 alituambia “kila mmoja aishi kwa urefu wa kamba yake”, tulipokuwa na madai ya fedha zetu kama waliyonayo hawa vijana wa mwaka walugha (2007-2008).

Ndugu zangu machozi yalinilenga lenga niliposikia hayo maneno ya aliyekuwa muwakilishi wa Rais wa Tanzania nchini Urusi, yaani Mh. Balozi, kwani ikumbukwe kuwa familia zetu ni duni pia huku Urusi ni mbali na nyumbani na hatuna kaka,mjomba, mama mdogo wala shangazi.

Inamaana mimi kama ni mtoto wa maskini niendelee kunyanyasika tu kwasababu wazazi wangu kamba zao ni fupi? Hatuwezi tukalijenga taifa letu kwa misingi hii ya matabaka.

Kama serikali yetu inashindwa kutuhudumia basi isingetuleta ughaibuni ili tuje tuteseke. Ingetuacha nyumbani ili maisha yakiwa magumu turudi majumbani tukale mlenda pamoja na wazazi wetu kwa sababu kamba zetu ni fupi..

Baada ya maisha kuwawia vigumu vijana hawa wa mwaka wa lugha (2007-2008) kama nilivyo elezea awali waliamua kwenda ubalozini kujua mustakabali wao lakini walifungiwa katika chumba kidogo cha mapokezi nje kukiwa kumetanda askari zaidi ya 30 na bila hata nafasi ya kwenda kujisaidia walikaa siku mbili mfululizo bila maji wala mkate , siku ya tatu wawakilishi kutoka wizara ya mambo ya nje ya Urusi walifika ubalozini na kushangazwa sana na kufungiwa kwa vijana hawa.

Wakamwamuru Balozi mlango ufunguliwe na vijana wapewe chakula ndipo hayo yakatendeka. Jamani watanzania, hii hainiingii akilini, kwamba warusi ambao mtaani wanatutemea mate na kututia manundu wanatuonea huruma ilhali ubalozi pamoja na wizara yetu wanaamua kutoa adhabu za jeshini ili kuwafunga wanyonge midomo?
Na baada ya hapo wanatoa taarifa za uongo kuwa wanafunzi wameuteka ubalozi, huo ni uongo wa kupindukia na sio ubinadamu wala uongozi wa sheria (rule of law). Kama serikali yetu inavyosema, kumnyima mtu chakula, maji , pamoja na kumfungia mlango asitoke hata kwenda chooni ni ukiukwaji wa utawala bora na haki za binadamu.

Naomba tulielewe hilo , sasa kuvamia na kuuteka ubalozi kuko wapi? Mimi kama rais wa wanafunzi ninasema madai ya vijana ni yakweli na ni haki yao, nitasimamia upande wao kwani penye ukweli uongo hujitenga , ninaiomba wizara yetu ya Elimu iangalie upya msimamo wake kuhusu madai haya kwani utaratibu wa wizara hauwezi kubadilishwa mwaka hadi mwaka kwa ajili ya kuwakandamiza wanyonge huku mafisadi wakiendelea kuzitumbua kodi za walala hoi.
Bado tunamatatizo mengi sana ambayo yanahitaji kuungwa mkono na watanzania wote wanaoijali na kuipenda nchi yao kama sisi.

Watanzania wenzangu, naomba niwaeleze kuwa fedha za kujikimu ambazo tunapewa kwa mwezi kiasi cha 292 US dollors , ni kidogo sana kutokana na ukweli kuwa hizo fedha matumizi yake ni

1.kulipia gharama za hostel(malazi) kiasi cha 840 us dollors kwa mwaka
2.fedha za chakula kwa kipindi chote cha mwaka mzima


3.fedha za vifaa vya masomo(stationery allowance)


4. fedha za practicals na field works kwa baadhi ya kozi.


5.fedha za kununulia madawa kwani bima ya afya hailipii madawa


6. fedha za usafiri kwamfano wengi wa wanafunzi husoma eneo lililopo mbali na hostels hii inamaanisha wanatumia usafiri wa basi na baadaye treni za umeme(metro) kwenda na kurudi kilasiku.

7. fedha za usajili(registration)

Ikumbukwe kuwa dola imeshuka thamani na inazidi kushuka thamani mwaka hadi mwaka kwani tulivyofika 2005 dola 1 ilikuwa sawa sawa na rouble ya Urusi 30 lakini kwa sasa dola 1 ni rouble ya urusi 22.45.

Hii inamaanisha kuwa, unapozibadili dola kwenda katika Roubles, thamani ya fedha inashuka. Naomba niwape mfano rahisi sana wa kupanda kwa gharama za maisha , mfano wakati tumefika mwaka 2005, mkate ulikuwa ukiuzwa rouble za urusi 10 lakini kwa sasa mkate unauzwa rouble za urusi 20.

ni ongezeko la asilimia 100 , nikisema tunapewa dola 292 unaweza ukafikiri ni fedha nyingi sana lakini mchanganuo nilioutoa hapo juu unaonyesha ni fedha ndogo sana kwa maisha ya kilasiku, ninauliza nani atatuokoa na kutunasua kutoka katika balaa hili?

Kama Serikali yetu ina nia thabiti ya kuwasomesha wanafunzi wengi nchini Urusi, Kwa nini isiwapeleke katika miji mingine tofauti na Moscow ambako gharama za maisha ziko chini?

Ninawaomba watanzania wenzetu mtusaidie katika mapambano haya magumu kwani bila msaada wenu mafanikio kwetu wanyonge wa Urusi pamoja na wanyonge wa nyumbani ni ndoto. Ninaahidi kusema ,kuzungumza,na kusimamia ukweli mpaka mwisho wa maisha yangu, kwani naamini ipo siku ukweli utafaamika na watanzania watatutetea na kutunasua kutoka katika janga hili kwani taifa imara la kesho lazima tuliandae leo.
Ni mimi
BONIPHACE –ELPHACE-MAGINA ,
RAIS wa umoja wa wanafunzi wa kitanzania
CHUO KIKUU CHA URAFIKI(PATRICE-LUMUMBA) MOSCOW
URUSI

No comments: