Monday, August 11, 2008

Jumuiya ya Watanzania Japan
Yapata Uongozi
Mpya...
Viongozi wapya wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Japan jana Jumapili wameitisha mkutano wao kwanza wa Watanzania wote kujadili mambo mbali mbali yanayohusiana na Jumuiya ya Watanzania hapa Japan pamoja na kujaza nafasi za mweka hazina wa Jumuiya na makamu wake na wajumbe wa kamati mbali mbali.


Viongozi hao wapya wa Jumuiya Dr.Ally Yahaya Simba(mwenyekiti),Bw. Andrew Kapinga (makamu mwenyekiti),Bw.Julius Mwombeki(katibu mkuu),Bw.Abby Senkoro(naibu katibu mkuu)walichaguliwa katika mkutano mkuu wa Watanzania wote uliofanyika tarehe 27 Julai 2008.Katika mkutano wa jana wajumbe waliwachagua Bw.Juma Kipaya(mweka hazina)na Bi. Fatma Mbilili(naibu mweka hazina).

Pia katika mkutano wa jana uliofanyika huko Odakyu Sagamihara,Kanagawa uongozi mpya wa Jumuiya uliwasilisha ripoti kuhusiana na makabidhiano ya fedha za Jumuiya kutoka kwa uongozi uliopita.Taarifa hiyo imeeleza kutoridhishwa kabisa na fedha taslimu pamoja na mchanganuo wa mapato na matumizi ya fedha za Jumuiya waliokabidhiwa na uongozi uliotanguliwa wengi wao wakiwa tayari wamerejea nyumbani au wamehama Japan.

Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya Dr.Ally Simba amewataka wanachama wasiwahukumu viongozi hao walioondoka madarakani kabla ya kupata taarifa na maelezo kamili.Ameahidi kuwa atawasiliana na viongozi wote walioondoka madarakani kuwataka watoe maelezo ya kina kuhusiana na fedha za Jumuiya.Aidha emeongeza kuwa atatoa muda wa kutosha kulingana na mazingira ili viongozi hao waliondoka madarakani wawasilishe maelezo na atachukua hatua zinazofuata kulingana na maelezo yatakayotolewa.

No comments: