Tuesday, August 5, 2008

jk atoa rambirambi ajali ya basi mbeya
SALAMU ZA RAMBIRAMBI ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE KUTOKANA NA AJALI YA BASI MKOANI MBEYA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. John Mwakipesile kutokana na ajali mbaya ya barabarani iliyosababisha vifo vya watu 10 na kujeruhi wengine 30 katika Mkoa wa Mbeya.

Ajali hiyo iliyohusisha basi la Kwitumba Line na Lori la Kampuni ya Dhandoo iliyotokea jana (Jumapili, Agosti 3, 2008) katika kijiji cha Senjele mkoani Mbeya.

“Nimesikitishwa sana na jinsi maisha ya watanzania wenzetu yanavyondelea kupotea katika ajali za barabarani. Napenda kwa dhati kabisa kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa watu 10 waliopoteza maisha yao katika ajali ya basi la Kwitumba Line na namwomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi Amin,” ameeleza Rais katika rambirambi hizo.

Ameongeza Rais: “ Naomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na nawaombea waliojeruhiwa kupona haraka ili warejee katika maisha ya kawaida. Mwenyezi Mungu awape imani na subira katika kipindi hiki kigumu na huku tukiwaombea ndugu zetu, mapumziko mema peponi.”

Aidha Mheshimiwa Rais amezitaka mamlaka zote zinazohusika na masuala ya usalama barabarani kuimarisha jitihada za kuhakikisha kwamba wasafirishaji wa abiria na mizigo wanazingatia kikamilifu sheria za usalama barabarani na kuwa makini zaidi na usalama wa vyombo wanavyoviendesha, ili kuepusha ajali zinazoendelea kupoteza maisha ya watu na uharibifu wa mali hapa nchini.

Amina.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

04 Agosti, 2008

No comments: