Tuesday, August 19, 2008

Balozi Ferdinand Ruhinda M/kiti
Mpya Bodi Ya TBC..
--------
RAIS Jakaya Kikwete amemteua Balozi Ferdinand Ruhinda kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Shirika la Utangazaji Tanzania(TBC).Taarifa ya Wizara ya Habari,Utamaduni na Michezo iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam imesema kuwa uteuzi huo umeenda sambamba na uteuzi wa wajumbe saba wa bodi hiyo uliofanywa na waziri wa wizara hiyo George Mkuchika.

Ruhinda amewahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za China, Thailand, Cuba na Canada.
Uteuzi huo wa mwenyekiti huyo na wajumbe wake,unafuatia marekebisho ya Sheria iliyofuta Taasisi ya Utangazaji Tanzania(TVT)na kuanzishwa kwa TBC kwa Tangazo la serikali namba 186 la Julai mosi 2007 chini ya sheria ya mashirika ya umma ya mwaka 1992.

Wajumbe wa bodi hiyo itakayomaliza muda wake Machi 13 mwakani ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu,Salvator Rweyemamu,Mkurugenzi wa Idara ya Habari(Maelezo) Kassim Mpenda,Dk Robert Mgombelo,Profesa Mwajabu Possi,Dominic Mahundi,Agnes Bukuku na Hassan Mitawi.
TBC imeanzishwa na serikali mwaka jana na majukumu yake ni pamoja na kutoa huduma bora na sahihi za utangazaji wa redio na televisheni kwa wananchi,kueneza usikivu wa redio na televisheni nchi nzima na kutangaza kutoka sehemu yoyote duniani kwa maslahi ya Watanzania.

No comments: