
Bado tunakukumbuka
Mwaka sasa umepita, bado tunakukumbuka,
Machozi hatujafuta, bado tunahuzunika,
Jina bado twaliita, kumbe ulishatutoka,
Bado tunakukumbuka, rafiki yetu Amina.
Ni vigumu kuamini, kuwa ilishatokea,
Machungu tele moyoni,vigumu kuyazowea,
Haupo tena duniani, mbali umeelekea,
Bado tunakukumbuka, rafiki yetu Amina.
Ni kama utani vile, ua letu kunyauka,
Nakumbuka siku ile, kichwani haitotoka,
Umekwenda zako kule, mwisho wako ‘ulipofika,
Bado tunakukumbuka, rafiki yetu Amina.
Amina mpiganaji, mahiri wetu vijana,
Nasi tulikutaraji, ‘ungetusaidia sana,
Mambo yetu kuyahoji, majibu kupatikana,
Bado tunakukumbuka, rafiki yetu Amina.
Uliacha changamoto, kwenye timu ya taifa,
Sasa imepamba moto, yacheza kwa maarifa,
Na sasa tunayo ndoto, itat’uongezea sifa,
Bado tunakukumbuka, rafiki yetu Amina.
Bunge uliloliacha, sasa kumepambazuka,
Kwa hakika kumekucha, hoja zinajadilika,
Kwa mafisadi kwachacha, kwao moto unawaka,
Bado tunakukumbuka, rafiki yetu Amina.
Ila vita ya madawa, bado inasuasua,
Ingawa wanaelewa, moyoni ‘ilikusumbua,
Dhati kwao haijawa, bado hawajatatua,
Bado tunakukumbuka, rafiki yetu Amina.
Amina dada Amina,rafiki yetu wa kweli,
Kama ingewezekana, kulitenda jambo hili,
Basi tungeomba sana, uturejee kimwili,
Bado tunakukumbuka, rafiki yetu Amina.
Kimwili haupo nasi, kiroho tupo pamoja,
Ni kweli tunakumiss, tutakuwona siku moja,
Familia yakumiss, Mungu aipe faraja,
Bado tunakukumbuka, rafiki yetu Amina.
Naweka kalamu chini, bado sisi twakupenda,
Upumzike kwa amani, mahali ulipokwenda,
Mahala pema peponi, malaika akulinde,
BADO TUNAKUKUMBUKA, RAFIKI YETU AMINA.
Ewe mdau Fadhili, asante we kwa shairi,
Nakuomba tafadhali, uniweke mstari,
usio mshahadhali, katika hili shauri,
Amina twamkumbuka, masikini na tajiri.
Twamkumbuka Amina, tajiri na masikini,
Na la kufanya hatuna, aliyopanga manani,
Anatajwa kila kona, kwamba awekwe peponi,
Amina twamkumbuka, masikini na tajiri.
Na siku zaenda mbio, kama vile ni utani,
Toka saa za machweo, hadi muda wa jioni,
Twaendeleza vilio, wapi Amina jamani,
Amina twamkumbuka, masikini na tajiri.
Hakika sikunuia, kukushukushuru globuni,
Mradi imetokea, acha na mie nighani,
Uchungu umegusia, ulotukaa moyoni,
Amina twamkumbuka, masikini na tajiri.
Kuna waliosahau, mwezi huu alitutoka,
Asante kwa yako mbiu, muda huu muafaka,
Ye si wa kumsahau, watu wa kila tabaka,
Amina twamkumbuka, masikini na tajiri.
Globu yako e fadhili, nimepita kwa yakini,
sikuona ufedhuli, ulojaa duniani,
Haki utafika mbali, kama si leo mwakani,
Amina twamkumbuka, masikini na tajiri.
Kaditama ninaomba, leo nikomee hapa,
Nikizidi kukuomba, daima usiwe kapa,
Endelea kaza kamba, usije ishia hapa,
Amina twamkumbuka, masikini na tajiri.
Salamu zangu za mwisho, mlio kama Fadhili,
Twahitaji burudish0, katika hapa pahali,
Kama hakuna mipasho, hapa ni penu mahali,
Amina twamkumbuka,masikini na tajiri.
- Kadidi-