Tuesday, April 29, 2008

Rostam Azizi alishitaki Gazeti la Mwana Halisi..


MFANYABIASHARA maarufu nchini,Rostam Azizi Pichani,amemshitaki Mhariri wa gazeti la kila wiki la MwanaHalisi na wachapishaji wake akitaka alipwe Sh bilioni tatu kwa kuchapisha habari zinazomkashifu zikimhusisha pamoja na mambo mengine, kashfa ya Kampuni ya Richmond.
Rostam ambaye pia ni Mbunge wa Igunga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amefungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wiki iliyopita, akimtumia wakili Kennedy Fungamtama. Licha ya kutaka alipwe kiasi hicho cha fedha, Mbunge huyo pia anaiomba Mahakama kutoa amri ya muda kulizuia gazeti hilo, wakala wake au yeyote kuchapisha habari zinazomkashifu.
Zaidi ya hayo, mfanyabiashara huyo ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Kamati Kuu, anaiomba Mahakama iliamuru gazeti hilo kumwomba radhi kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti hilo kwa uzito uleule au zaidi baada ya hukumu yake.
Pia anaomba alipwe gharama za kesi. Rostam anadai kuwa gazeti hilo la MwanaHalisi lilichapisha habari za uongo na za kumkashifu katika toleo lake namba 084 la Februari 13 hadi 19, mwaka huu, chini ya kichwa cha habari, “Richmond ya Rostam Azizi, Ndiye aliyeileta nchini.” Kulingana na mfanyabiashara huyo, kichwa hicho cha habari pamoja na habari yenyewe, zinaonyesha kuwa yeye ni mdanganyifu, asiye mwaminifu, mtoa rushwa na anayetenda matendo maovu na mtu anayeshiriki katika mambo ya udanganyifu.
Rostam anadai kuwa licha ya kuweza kupatikana kwa taarifa sahihi na za wazi kwa urahisi na kwamba kwa njia yoyote ile hajashiriki katika matendo hayo maovu, gazeti hilo liliendelea na kampeni chafu dhidi yake katika toleo lake la 085 la Februari 20 hadi 26, mwaka huu. Anadai kuwa gazeti hilo linadaiwa kuchapisha habari nyingine kwenye ukurasa wa pili chini ya kichwa cha habari, “Kikwete amtosa Lowassa” likimhusisha na biashara zake na kampuni yake, kwamba ni mtu anayefahamika kwamba anaweza kubadilisha ukweli kukidhi matakwa yake.
Mbunge huyo analituhumu gazeti hilo kuendelea kuchapisha habari kama hizo katika toleo lake la 087 la Machi 5 hadi 11, mwaka huu na toleo la 093 la Aprili 16 hadi 22, mwaka huu likimwonyesha kuwa si mtu muadilifu na anatumia vibaya nafasi yake kwa maslahi yake binafsi. Mfanyabiashara huyo analalamika kuwa maneno hayo yalikuwa na nia ya kumchafua katika biashara na kazi yake kama Mbunge; hivyo kuharibu wasifu, tabia, uadilifu na hadhi yake na kuonyeshwa kwenye jamii kuwa ni mtu wa kashfa, asiye na maana na mdanganyifu.
Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, amejijengea hadhi kama raia mwema, mfanyabiashara, mwanasiasa na mtu wa kuaminika kwa miaka mingi na kutokana na kashfa hiyo, amevunjiwa hadhi mbele ya jamii. Mbunge huyo amedai kuwa anastahili kulipwa kutokana na udhalilishaji huo kwani hadhi yake imeshushwa kiasi cha kuathiri biashara na kazi yake kwa kiwango cha kushindwa kuendesha kazi na biashara yake kwa urahisi.Habari hii na Faustine Kapama.Picha na Salum Mnette

No comments: